31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JKCI yasaidia asilimia 85 wagonjwa wa moyo kutibiwa nchini

Na AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM

MKURUGENZI Mtendaji wa taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk. Mohamed Janabi, amesema taasisi hiyo imesaidia asilimia 85 ya wagonjwa wa moyo kutibiwa ndani ya nchi, huku asilimia 15 wakisafirishwa nje.

Akizungumza wakati wa ziara iliyofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika taasisi hiyo jana, alisema kutibiwa kwa wagonjwa wa moyo ndani ya nchi ni hatua kubwa ya mafanikio kwani awali matibabu hayo yalikuwa yanapatikana nje ya nchi.

“Kuna mafanikio makubwa sana hapa nchini, kwa kuanzishwa taasisi hii wagonjwa wengi wa moyo sasa wanatibiwa humu ndani, wamefikia asilimia 85, haya ni mafanikio ya kiwango kikubwa kwani mwanzoni wagonjwa wa moyo walikuwa wanasafirishwa kwenda India, lakini sasa wanatibiwa ndani ya nchi,” alisema Dk. Janabi.

Alisema kati ya wagonjwa waliolazwa asilimia 8.7 ndio wanaopoteza maisha huku akitaja asilimia kubwa wanaougua ugonjwa wa moyo ni umri kuanzia miaka 15 hadi 63.

“Asilimia ya wagonjwa 8.7 kati 10,000 waliolazwa kwa kipindi cha miaka mitatu ndio walipoteza maisha, hata hivyo hospitali ina miundombinu licha ya gharama kubwa ya matibabu inayofikia hadi Sh milioni 10.

“Idadi ya wanaofanyiwa upasuaji kwa wiki moja inaweza kufikia 6 hadi 10, pia tuna uwezo wa kuhudumia watoto 40 kwa siku, asilimia 42 ya umri chini ya miaka 15 wanaougua moyo, huku asilimia 55 wa umri kati ya 15 mpaka 63 wanaougua moyo, hii ndio idadi kubwa ya watu wanaougua,” alieleza Dk. Janabi.

Alisema wanaendelea kufanya upasuaji wa kisasa wa kutibu magonjwa ya moyo bila kufanya upasuaji kwa mgojwa, hivyo kadiri siku zinavyoenda wanapata teknolojia mpya.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda aliitaka jamii kujitokeza kutoa misada kwa watu wasiokuwa na uwezo.

“Watoto hawa wanahitaji msaada wa jamii, ukimsaidia leo Mungu naye atakulipa siku zijazo, kwahiyo ninawaomba Watanzania wawasaidie watu wenye uhitaji bila kujali au kusubiri kulipwa,”alisema Makonda.

Ziara hiyo ni mwendelezo wa kuwasaidia watoto kumi kwa kila mwezi wanaoungua ugonjwa wa moyo, ambapo kwa mwezi huu amewasaidia watoto 10 kutoka sehemu mbalimbali nchini.

Mmoja wa wazazi, Tarsila John alisema wanafurahi huduma wanazopata katika hospitali hiyo  kwani sasa mtoto wake anaendelea vizuri.

“Nilimleta mtoto wangu wa miezi miwili akiwa na hali mbaya, lakini sasa anaendelea vizuri na tunafurahia huduma za hapa, tunaomba watu wawe na moyo wa kutusaidia kwani watu wengi hapa ni wahitaji, wengine wametoka mikoa ya mbali,” alisema Tarsila.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles