25.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

JKCI yaja na mpango kwa wenye selimundu

Aveline Kitomary -Dar es salaam

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imezindua programu mpya ya kliniki kwa wagonjwa wenye selimundu (sickle cell) ambao wanapata matatizo ya moyo ili kuweza kurahisisha matibabu yao.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa taasisi hiyo ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Profesa Mohammed Janabi, alisema kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Kishiriki cha Muhimbili (Muhas) wameweza kuwaunganisha programu hiyo.

Profesa Janabi alisema kwa kawaida wagonjwa wa selimundu huwa wana uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo, hii ni baada ya damu kuwa pungufu na kufanya   moyo kupiga haraka zaidi ili uweze kuzungusha damu.

“Tumekuwa tukijaribu kuanzisha hii programu kwa miaka miwili sasa, na dhumuni kubwa ni kwamba kama mnavyofahamu selimundu anazaliwa nayo mtu na ugonjwa huo huweza kufanya kupata matatizo ya moyo pia. 

“Kilichokuwa kinatokea huko nyuma ni kwamba kunakuwa na kliniki ya Muhas inayofanyika Hospitali ya  Muhimbili na wakigundua mgonjwa ana tatizo  la moyo, anaambiwa aje hapa kwenye taasisi  kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya kuonwa.

 “Tarehe anaweza kupangiwa mwezi mmoja hata miwili, tukashauriana sisi kama madaktari na wataalamu wa programu  ya  Muhas,  kwamba haya magonjwa yanaingiliana kwanini tusifanye  kliniki moja akawepo daktari wa moyo na atakuwepo daktari wa selimundu na vipimo vitafanyika kwa siku moja anapokuja mgonjwa,” alieleza Profesa Janabi.

Alisema kwa sasa vipimo vyote vitafanyika sehemu moja, hivyo itapunguza muda wa matibabu.

 “Watafanyiwa vipimo vyote vya moyo, damu na dawa kutolewa itawarahisishia, badala ya kwenda kwenye kliniki mbili na kwa siku mbili tofauti watapata huduma sehemu moja.

“Dhumuni kubwa ifike siku yale magonjwa yanayoingiliana kuwe na kliniki moja ambayo mgonjwa  wa figo na moyo ambaye ana matatizo yote mawii au moyo na kisukari watibike kwa siku moja na sehemu moja,” alisema Profesa Janabi.

Alieleza kuwa matibabu ya sehemu moja itasaidia  wataalamu kuweza kujadiliana ili kuweza kutoa huduma haraka.

“Kwamba tumeona hapa kuna sickle cell, lakini imefanya moyo kuwa mkubwa, kuharibu valvu, tunaamua nini cha kufanya, tukifanya upasuaji tukamaliza au kutoa dawa bado anaendelea na kliniki.

 “Karibia kila siku tunaona mgonjwa wa sickle cell mwenye magonjwa ya moyo na tunaendelea kuandaa takwimu baada ya miezi miwili, lakini ikifikia hatua ya kufanya kliniki tatizo lipo,” alibainisha Profesa Janabi.

Alishauri wagonjwa kuweza kuhudhuria kliniki na kufuata maelekezo ambayo wanaelekezwa na wataalamu wa afya wanaowahudumia. 

 “Wagonjwa wa sickle cell wana masharti ya kuishi na dawa zao za kinga na kuhudhuria kliniki na kufuata maelezo,” alisema Profesa Janabi.

Alisema taasisi yao inatoa msaada wa matibabu ya bure kwa mwezi kuanzia Sh milioni 120 hadi 150, hivyo ni muhimu kwa kila mwananchi kuwa na bima ya afya.

“Kuhusu gharama hazikwepeki, lakini tunawashauri watu kuwa na bima kwa sababu dawa ziko kwenye bima kama tunavyofanya kwa magonjwa ya moyo, lakini kwa wale ambao hawana uwezo kuna taratibu zetu na kutoa msamaha,” alishauri Profesa Janabi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,444FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles