24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

JKCI YAFANYA UPASUAJI KUZIBUA MISHIPA YA DAMU

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WAGONJWA 37 wamefanyiwa upasuaji wa kuzibua mishipa ya damu katika moyo iliyokuwa imeziba kabisa na hivyo kusababisha damu kushindwa kusafiri sehemu mbalimbali za miili yao.

Upasuaji huo umefanyika katika Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) tangu Januari mosi, mwaka huu hadi kufikia juzi.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI, Tulizo Shemu, alisema wagonjwa wote hali zao zinaendelea vizuri na wengine wamesharuhusiwa kurejea nyumbani.

“Wagonjwa hawa tumewafanyia upasuaji wa kuzibua moyo pasipo kufungua kifua katika mtambo wetu maalumu wa ‘cath lab’ kwa kushirikiana na madaktari wenzetu wa Taasisi ya Madaktari Afrika kutoka nchini Marekani,” alisema.

Alisema tatizo la kuziba mishipa ya damu katika moyo linawakabili watu wengi hivi sasa na kwamba hiyo ni kutokana na mfumo mbovu wa maisha.

“Ulaji mbovu, kutokufanya mazoezi ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuziba kwa mishipa ya damu,” alisema Dk. Tulizo.

Akizungumzia kambi ya matibabu iliyoanza Januari 23 hadi 25, mwaka huu hospitalini hapo, Mkurugenzi wa Idara ya Tiba wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, alitaja changamoto kubwa waliyokabiliana nayo kuwa ni upatikanaji wa vifaa.

“Tumeweza kuzibua mishipa kwa kiwango cha asilimia 100 tofauti na awali tulikuwa tukiishia asilimia 70 hadi 80, tofauti na kambi nyingine tulizowahi kufanya ambazo tulikabiliwa na uhaba wa damu, awali hii upatikanaji wa vifaa ndiyo changamoto tuliyokabiliana nayo.

“Hawa wenzetu (suppliers) wengi wanashindwa kuleta vifaa kwa wakati, nchi yetu ina uhaba wa wataalamu wa moyo pia, kwa hiyo ili kukabiliana na hali hiyo, tumeanza kutoa mafunzo kwa wale wanaosoma ‘masters in science’, tunaamini baada ya muda fulani idadi ya wataalamu itaongezeka,” alisema.

Naye Dk. Patin O’Brien wa Taasisi ya Madaktari Afrika, alisema wataendelea kushirikiana na JKCI kuwapa mafunzo madaktari wake ili wazidi kubobea zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles