Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeeleza kuwa matarajio yao ya miaka mitano ijayo ni kupandikiza moyo kwa watu wenye umri mbukwa ambao moyo wao umechoka kufanya kazi.
Akizumgumza leo Julai 18, jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge amesema Taasisi hiyo ni hospitali maalumu inayotoa tiba ya magonjwa ya moyo, mafunzo na utafiti.
“Miaka mitano ijayo tunatarajia tuwe tunapandikiza moyo, lazima kuwe na maandalizi ya sheria itapitiwa ili watu waweze kujitolea moyo kama mtu amepata ajali uwezekano wa kupona haupo au mgonjwa yupo mahututi hawezi kupona anaweza kusema tuchukue moyo utamsaidia mtu mwenye uhitaji wa moyo kama hauna shida yoyote ili aendelee kuishi,” amesema Dk. Kisenge.
Amesema bado kuna ongezeko la magonjwa yasiyoambukizwa lakini ugonjwa wa moyo unaongezeka kwa kasi na unasababisha watu kupoteza maisha kutokana na mfumo wa maisha uliopo.
Amesema unaweza kuepuka magonjwa ya moyo kwa kufanya mazoezi kwa wiki mara tatu na kwa muda wa nusu saa, kuzingatia. Lishe bora, kuepuka uvutaji sigara na unywaji pombe uliokithiri.
“Kutambua kiwango cha sukari katika mwili wako, kutambua msukumo wa damu na kiwango cha mafuta mwilini na kupima afya ya moyo japo mara moja kwa mwaka kunaweza kukusaidia kujua kama una tatizo hili au kama unatatizo kupatiwa matibabu mapema,” amesema Dk. Kisenge.
Amesema katika mwaka wa fedha uliopita 2022 /23 JKCI ili tengewa bajeti ya Sh bilioni 44.5 ambazo zilitumika katika shughuli mbalimbali za sekta ya afya.
Aidha, Dk. Kisenge amesema kwa mwaka wa fedha 2023/24JKCI imetenga bajeti ya kiasi cha Sh bilioni 66.2 na kwamba fedha hizo zitatumika kwenye utekelezaji wa kazi na mipango mbalimbali.
Ametaja mipango kuwa ni kuimarisha tiba moyo kwa kudhamini masomo ya muda mfupi na mrefu, kununua vifaa tiba vya kisasa zaidi, kuendeleza ujenzi mbalimbali, kutoa huduma za tiba mkoba kwa kuwafuata wananchi waliopo mikoani wanashinda kufika Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa manufaa ambayo wananchi watapata kupitia vipaombele vya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha huu ni kukamilika kwa jengo la utawala na vipimo lililogharimu Sh bilioni 3.6.
“Kutasaidia wagonjwa wengi zaidi kupata huduma za vipimo vya moyo kwa wakati pia wafanyakazi watakuwa na ofisi za kutosha na hivyo kupunguza msongamano. Katika ofisi walizopo sasa,” ameeleza Dk. Kisenge.
Amesema kabla taasisi hiyo haijaanzishwa, kwa mwaka wagonjwa walikuwa wanapelekwa kutibiwa nje ya nchi kwa gharama ya Sh bilioni 62.3.
“Tangu taasisi hii ianzishwe na uwekezaji wa Serikali kwa mwaka matibabu ya wagonjwa wa moyo gharama yake ni Sh bilioni 31, tunaweza kuokoa Sh bilioni 31 ambazo zilikuwa zinapotea kupeleka wagonjwa nje ya nchi,” amesema Dk. Kisenge.
Akizungumzia kuhusu wagonjwa kutoka nje ya nchi amesema kipindi cha mwaka mmoja wagonjwa waliotibiwa katika taasisi hiyo kutoka nje ya nchi walikuwa 301 kupitia wagonjwa hao walipata kiasi cha fedha milioni 200.
Amesema wataendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu magonjwa ya moyo kwa kupitia vyombo habari na amewasisitiza waendelea kufanya mazoezi na kufuata lishe bora ni muhimu.