27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JKCI kuwasilisha tafiti saba za moyo kwa wanasayansi

Ales Mbilinyi – JKCI

TAFITI saba za magonjwa ya moyo zilizofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), zinatarajiwa kuwasilishwa  katika mkutano wa wanasayansi, madaktari bingwa na wahudumu wa afya wanaotoka nchi za ukanda wa Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika utakaofanyika wiki ijayo nchini Zambia.

Tafiti hizo ambazo zimefanyika mwaka jana na mwaka  huu, ni kuhusu  mwenendo wa mapigo ya moyo kwa mgonjwa, wagonjwa wenye moyo ambao uwezo wake wa kufanya kazi umepungua  jinsi wanavyozingatia matibabu kama walivyoshauriwa na madaktari, shinikizo la damu na tatizo la kisukari.

Nyingine ni upungufu wa nguvu za kiume katika jamii, uelewa wa sababu hatarishi za magonjwa ya moyo katika jamii,  magonjwa matatu kwa pamoja yaani moyo na figo kushindwa kufanya kazi  na upungufu wa damu mwilini.

Akizungumza kuhusu tafiti hizo, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa JKCI, Dk. Pedro Pallangyo, alisema tafiti hizo zimefanyika Mkoa wa Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka miwili na kwa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo.

 “Tumekuwa tukifanya tafiti mbalimbali kuhusu magonjwa ya moyo ambazo zinatusaidia kufahamu wagonjwa wetu pamoja na wananchi wanaotuzunguka wanakabiliwa na matatizo gani katika afya za moyo na hii inatusaidia kuweza kuboresha huduma zetu,” alisema.

Kuhusu mkutano huo wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Dk. Pedro alisema kwa upande wa magonjwa ya moyo utawasaidia  kubadilishana matokeo ya huduma za matibabu wanazozitoa, hasa tafiti zinazofanywa katika nchi mbalimbali  ili kuboresha huduma zinazotolewa kwa wagonjwa.

Ofisa Uuguzi wa JKCI, Jalack Milinga, ambaye alishiriki kufanya tafiti hizo, alisema  kwake ni mara ya kwanza kuhudhuria mkutano huo ambao utamsaidia kuongeza ujuzi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa moyo, lakini pia kubadilishana uzoefu na wauguzi wenzake watakaoshiriki.

“Utafiti wangu uliangalia jinsi ya uzingatiaji wa unywaji wa dawa za moyo kwa wagonjwa ambao mioyo yao haifanyi kazi vizuri.

“Hivyo naamini ushiriki wangu katika mkutano huu utaniwezesha kupata mbinu mpya za kusimamia  jukumu  la kuwasaidia wagonjwa wetu kuzingatia matibabu ili kupata matokeo bora ya tiba,” alisema Milinga.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI, Smita Bhalia, alisema ushiriki wa wataalamu kutoka Tanzania  umelenga kutoa matokeo ya utafiti uliofanywa hapa nchini na kuonyesha baadhi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza jinsi yanavyoweza kusababisha magonjwa ya moyo ama magonjwa ya moyo yanavyoweza kusababisha mtu kupata magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza.

Malengo ya mkutano huo ni kwa nchi  washiriki kutoka  ukanda wa Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika kuona  jinsi ya kushirikiana katika kufanya tafiti za ndani, kuwa na  njia bora na za kisasa za matibabu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza  na kuwa na  mbinu mpya za kuweza kuzuia magonjwa hayo.

Mkutano huo ambao hufanyika kila mwaka, unatarajia kufayika mjini Livingstone, Zambia kuanzia Septemba 5 hadi 7. Mwaka jana ulifanyika Nairobi nchini Kenya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles