30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JKCI kufanya upasuaji moyo kwa wagonjwa 12

AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM

JUMLA ya wagonjwa 12 ambao mishipa yao ya damu ya moyo imeziba kwa muda mrefu, wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji unaohitaji utaalamu wa hali ya juu katika kambi maalumu ya matibabu inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam,  daktari bingwa wa moyo, mbobezi wa moyo na mzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa JKCI, Peter Kisenge alisema kambi hiyo ya siku tatu wanaifanya kwa kushirikiana na daktari kutoka nchini Saudi Arabia na Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani.

“Matibabu ya wagonjwa ambao mishipa yao ya damu imeziba na kukaa kwa muda mrefu bila ya kupata matibabu ni magumu na yanahitaji utaalamu wa hali ya juu. Kupitia kambi hii wagonjwa wenye matatizo hayo watapata matibabu,” alisema Dk. Kisenge ambaye pia ni mkurugenzi wa tiba ya moyo.

Alisema aina ya matibabu yanayofanyika ni ya kuzibua mishipa ya damu ya moyo kwa njia ya upasuaji mdogo wa moyo wa bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab ambapo mgonjwa anatobolewa tundu dogo katika mshipa wa damu wa mkono.

“Upasuaji wa aina hii una faida kubwa kwa mgonjwa kwani baada ya matibabu kukamilika anaweza kukaa hospitali kwa muda wa saa chache na kuruhusiwa kurudi nyumbani bila kulazwa wodini.

“Faida nyingine inayopatikana katika kambi hii ni utoaji wa mafunzo ambayo yatawawezesha madaktari kutoka JKCI kuendelea kutoa huduma hizi siku za mbeleni,” alieleza  Dk. Kisenge.

Aidha aliwaomba madaktari nchini kutuma wagonjwa waliopo mikoani wenye matatizo ya moyo, hasa wenye matatizo ya mishipa ya damu ya moyo iliyoziba ili waweze kupata matibabu sahihi katika taasisi hiyo.

Kwa upande wake, daktari mbobezi wa moyo na mzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo kutoka Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani, Eric Powers, alisema madaktari kutoka shirika hilo wamekuwa wakitoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wataalamu wa JKCI na sasa wanatoa  mafunzo ya uzibuaji wa mishipa ya damu iliyoziba kwa muda mrefu kupitia mishipa iliyopo kwenye mikono.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles