23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JKCI Dar Group ni kwa ajili ya matibabu ya watoto-Ummy

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Serikali imesema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kituo cha Dar Group (JKCI Dar Group) iliyopo Tazara jijini Dar es Salaam itahudumia watoto wenye matatizo ya moyo wenye umri chini ya miaka 15.

Agizo hilo la Serikali limetolewa leo Januari 14, 2023 na Waziri wa Afya,Ummy Mwalimu alipotembelea Hospitali hiyo ambayo sasa ipo chini ya usimamizi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.

Waziri Ummy alitoa uamuzi huo baada ya awali, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dk. Peter Kisenge la kutaka kukifanya kituo hicho kuwa kubobea katika utoaji wa huduma tofautitofauti za afya kwa wananchi wa rika zote.

“Nimesikiliza mapendekezo ya Mkurugenzi wa JKCI, Dk. Kisenge lakini hapa nataka tujikite kwenye matibabu ya moyo kwa watoto walio chini ya miaka 15 tusitoke kwenye huduma ya moyo kama ilivyokuwa malengo ya Taasisi ya Moyo JKCI.

“Rufaa zote za watoto wenye matatizo ya moyo zinatakiwa kuja hapa JKCI Dar Group badala ya Taasisi ya Moyo JKCI iliyopo Muhimbili ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika eneo moja wakisubiri huduma.

“Sote ni mashahidi kwamba hapa tulipo (JKCI Dar Group) tupo katika mazingira rafiki kufikika kwa wakazi wa Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni lakini hata kwa wageni wanaofika katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa usafiri wa treni au anga hivyo kuagiza Hospitali hiyo kuboresha zaidi huduma zinazotolewa ili kuvutia watu,” amesema Waziri Ummy.

Pamoja na agizo hilo Waziri Ummy amesema kuwa huduma nyingine mbali na matibabu ya moyo yataendelea kutolewa katika kituo hicho kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.
Katika hatua nyingine ameagiza taasisi hiyo kufunga vituo vyaka ya Morogoro na Mbeya nakwamba wafanyakazi hao warejeshwe Dar es Salaam ili kukipa uwezo kituo cha JKCI Dar Group.

Akimkaribisha Waziri Ummy, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumani Nagu ameipongeza Taasisi ya JKCI kwa kuipokea hospitali ya Dar Group kwa vitendo na kuanza maboresho ya huduma kwa haraka katika kipindi cha miezi miwili.

“Ni dhamira ya serikali kupambana na magonjwa yasiyoambukiza hivyo JKCI ina mchango mkubwa katika kutibu na kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, hivyo tutasogeza karibu huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo kwa wananchini,” amesema.

Prof. Nagu amesema pamoja na kupanua wigo wa huduma, Serikali itaendelea kuhimiza ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Itakumbukwa kuwa awali Hospitali ya Dar Group ilijengwa kwa ajili ya kutoa Huduma za Afya kwa wafanyakazi wa Viwandani na kusimamiwa na Msajili wa Hazina.

Novemba 2022 serikali kupitia Wizara ya Fedha, Msajili wa Hazina ilifanya maamuzi ya kuichukua Hospitali hiyo na kuipatia Wizara ya Afya kwa ajili ya usimamizi na kutatua changamoto za kiutendaji zilizokuwepo hapo awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles