Na ESTHER MNYIKA
-DAR ES SALAAM
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), inatarajia kupeleka mapendekezo bungeni kutunga sheria ya kuruhusu kuchukua figo na maini ya mtu aliyefariki kwa ajili ya kupandikiza kwa mtu mwingine.
Mkurugenzi wa Upasuaji wa JKCI, Dk. Bashir Nyangasa amesema utaratibu huo ambao umekuwa ukifanyika katika nchi nyingine duniani utasaidia kuokoa maisha ya watu wengine na kwamba taasisi hiyo ina uwezo wa kupandikiza viungo hivyo vya mwili kwa binadamu.
“Utaratibu huo kwa nchi za wenzetu upo na sheria zipo na mtu ana uwezo wa kusema kama nikifariki maini, figo na moyo vichukuliwe kwa kutiliana saini kama vitabainika havina tatizo lolote vitumike kwa kupandikiza.
“Kwa hapa nchini bado hatuna sheria hiyo hivyo tunarajia kupeleka mapendekezo Bungeni ili yatungiwe sheria,” amesema Dk. Nyangasa.
Hata hivyo, amesema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo wamefanya mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vinavyotokana na maradhi ya moyo kwa asilimia kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kwa mwaka 2016 wamefanya uchunguzi wa tiba kwa wagonjwa 973, ambapo kati ya hao 620 walipatiwa matibabu ya moyo ya bila kufungua kifua kwa kupitia mishipa ya damu kwa kutumia mtambo wa ‘Catheterization’.