22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

JK awananga wabaya wa CCM

Jakaya Kikwete

Na Bakari Kimwanga, Dodoma

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, hatimaye amewaaga wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho huku akiwananga watu waliokuwa wakikiombea dua mbaya chama hicho ili kife.

Amesema katika muda wote aliokaa madarakani kwa kipindi cha miaka 10, hali ilikuwa nzuri lakini kwa mwaka jana wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu kuna watu walidhani chama hicho kingekufa ili watume salamu za rambirambi na matokeo yake jaribio lake limeshindwa.

Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha Kamati Kuu (CC), ambayo ilikuwa na ajenda moja ya kupitisha jina la Rais Dk. John Magufuli aweze kuwania nafasi ya uenyekiti wa CCM.

Kikwete ambaye pia ni Rais mstaafu wa awamu ya nne, alisema anajisikia raha sana kuzungumza na wajumbe wa Kamati Kuu yake ya mwisho, ambao kwake walikuwa wakimsaidia kazi ya kukujenga chama wakati wote wa utawala wake.

“Raha sana leo (jana), haijapata kutokea maana hii ni Kamati Kuu yangu ya mwisho na bila msaada wenu CCM isingekuwa imara kama ilivyo sasa.

“Wako watu walidhani CCM ingekufa na walishajiandaa kwa ajili ya kutuma salamu za rambirambi. Pia wako waliodhani tutaumbuka sasa wameumbuka wao na jaribio lao limekwama kabisa na hawataweza tena,” alisema Kikwete

Alisema kikao hicho cha Kamati Kuu kitajadili ajenda moja ya kupendakeza jina la Rais Dk. John Magufuli, aweze kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM taifa.

Awali akizungumza kabla ya kufunguliwa kwa mktano huo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema wajumbe wanaotakiwa kuhudhuria CC ni 32 lakini waliopo ni 28.

“Wajumbe wa CC ni 32 na walihudhuria leo hii (jana) ni wajumbe 28 ambayo ni sawa na asilimia 87.5 hivyo akidi imetimia,” alisema Kinana

Hadi kikao hicho kinaanza wajumbe ambao hawakuonekana ukumbini ni pamoja na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, Spika wa Bunge, Job Ndugai na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai.

Hata hivyo wakati kikao hicho kinaanza hapakuwa na mjumbe yeyote wa Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM, linaloongozwa na Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi huku ikitarajiwa vigogo hao wastaafu kuwasili.

Mbali na Mwinyi wajumbe wengine ni  Pius Msekwa (Katibu) na wajumbe ni Rais mstaafu Benjamin Mkapa pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu (Bara), John Malecela.

Hata hivyo baraza hilo sasa linatarajiwa kupokea wajumbe wapya ambao ni Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana.

Nape apambana na maafisa usalama

Kabla ya kuanza kwa kikao cha CC, Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye alipambana na maafisa usalama ambao waliwazuia waandishi wa habari kuingia ukumbini kuhudhuria ufunguzi wa kikao hicho.

Nape aliwaeleza maafisa hao umuhimu wa waandishi wa habari kuingia ndani ya ukumbi kwa sababu shughuli ni ya CCM na si ya Serikali, ambapo maafisa hao walilegeza msimamo wao wa awali na kuwaruhusu wanahabari kuingia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles