Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS mstaafu Jakaya Kikwete jana aliwasili katika Mji wa Dubai na kumjulia hali Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Kikwete aliyekuwa safarini kuelekea nchini Canada alituma picha kupitia ukarasa wake wa Twitter akisalimiana na kiongozi huyo wa kiroho aliyeondoka nchini mwanzoni mwa Mei, mwaka huu na kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya matibabu.
“Nikiwa Dubai safarini kwenda Canada, nimemtembelea asubuhi hii Mhadhama Polycarp Kardinali Pengo na nimefarijika kumkuta akiwa na siha njema,” aliandika Kikwete katika ukurasa wake wa Twitter.
Hata hivyo, hadi sasa bado haijajulikana Pengo yupo nchini humo kwa ajili ya mapumziko ama matibabu baada ya taarifa ya awali kueleza kuwa alienda Marekani kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mwanzoni mwa Mei, mwaka huu na Askofu Msaidizi wa Jimbo la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, ilisema Pengo alisafirishwa Mei 2, mwaka huu kwa ajili ya kupatiwa matibabu na kufanyiwa uchunguzi.
Taarifa ilisema kuwa Pengo anatarajiwa kuwapo Marekani kwa mwezi mmoja.
“Tuendelee kumuombea Baba Kardinali Pengo ili Mwenyezi Mungu amjalie nguvu na afya njema ya mwili na roho ili aweze kuliongoza vema Taifa la Mungu alilokabidhiwa,” ilisema taarifa hiyo.
Hivi karibuni, hali ya afya ya Pengo ilionekana kudhoofu kutokana na maradhi yanayomsumbua kitendo kilichosababisha ashindwe kuongoza misa kanisani.