24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

JIWE LAPOROMOKA MLIMANI NA KUINGIA SEBULENI MWANZA

Na BENJAMIN MASESE-MWANZA

FAMILIA ya David Masanga, mkazi wa Mtaa wa Kishili B, Kata ya Kishili jijini Mwanza, imenusurika kufa baada ya jiwe kubwa kuporomoka kutoka mlimani na kuvamia nyumba yao.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 12 jioni ambapo ghafla jiwe hilo liliporomoka kutoka mlima ambao upo karibu na kubomoa ukuta na kuingia sebulani na kukandamiza vyombo vyote vilivyokuwamo.

MTANZANIA ilifika eneo la tukio na kushuhudia jiwe hilo likiwa limegota sebulani, huku vyombo vyote vya kupikia na samani vikiwa vimevunjika na kuta zilizobaki zikiwa na nyufa.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika eneo la tukio,  mmiliki wa nyumba hiyo, David Msanga, alisema wakati tukio linatokea alikuwa ametoka na mke wake, Magreth huku wakiwa wamewaacha watoto wao wawili.

“Tulipigiwa simu na majirani kwamba jiwe limevamia nyumba na kubomoa, tulikimbia kuja nyumbani tukiwa na hofu kubwa ya usalama wa watoto wetu, kwa bahati nzuri wakati jiwe hilo linaporomoka, watoto walikuwa nje wanaoga na waliliona linashuka ikabidi wakimbie.

“Chanzo cha jiwe hilo kuporomoka ni kwamba kulikuwa na mtu anapasua mawe huko juu kwa kutumia chenga za mkaa, inavyoonekana  lilivyopasuka lilishuka chini ghafla, baada ya tukio alikimbia.

“Kama unavyoona jiwe hilo limeharibu vitu vyote vilivyokuwa sebuleni na sehemu iliyobaki haipo salama tena. Kwa usalama wetu, tunaomba jamii na Serikali iweze kutusaidia kwa kipindi hiki ili tuweze kujipanga upya,” alisema.

Masanga alisema thamani ya vyombo vilivyoharibika ni zaidi ya Sh 300,000 huku nyumba ni zaidi ya Sh milioni moja. Pia aliwaomba uongozi wa mtaa kumsaidia namna ya kutoa jiwe hilo ndani.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kishili B, Buligu Kitambo, alisema licha ya chanzo cha jiwe hilo poromoka kuwa mpasua mawe, lakini mazingira ya wakazi wanaoishi chini ya mlima huo yapo shakani kutokana na mawe mengi kuwa na dalili ya kuporomoka.

“Nikiwa kama mwenyekiti wa mtaa huu, sijawahi kuidhinisha barua ya uuzwaji wa viwanja karibu na milima hatarishi kama hii, naomba wananchi mchukue tahadhari kwani mnaweza kupata madhara namna hii, katika hili naomba wananchi tujitolee kwa msaada wetu wa kutoa jiwe ndani,” alisema.

Mtendaji wa Kata hiyo, Salenda Mvanga, alisema eneo hilo ni hatari, hivyo aliagiza hatua za kumhamisha Msanga zianze haraka ili kuepusha athari nyingine.

“Binafsi nimekuwa nikitembea maeneo mbalimbali kutoa elimu juu ya kuwazuia kujenga mlimani, sasa madhara kama haya ndiyo hatutaki yatokee, hapa alipo hana kibali cha kujenga hapa na leo nasema tena ahame eneo hili ili akatafute sehemu salama,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles