Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
IDADI ya watalii wanaokuja nchini baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kushiriki na kuongoza ziara za uzinduzi wa filamu ya Royal Tour nchini Marekani imezidi kuongezeka ikilinganishwa na kabla ya uzinduzi huo.
Kwa wiki kadhaa sasa viwanja vya ndege, hoteli na mbuga za wanyama zimeshuhudia ongezeko hilo la watalii ambao hawajawahi kutokea nchini.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO), Christine Mwakatobe amesema watalii zaidi ya 1,700 kutoka Ulaya na Asia hushuka kila siku kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) na kwenda moja kwa moja katika hifadhi za taifa.
Mwakatobe amesema jana kuwa kwa siku hutua ndege tatu hadi tano kwenye kiwanja hicho kilichoko Kaskazini mwa Tanzania.
Amesema kila ndege hushusha watalii zaidi ya 300 na ukiachilia mbali ndege kubwa zinazotoka moja kwa moja Ulaya na Asia, pia KIA hutua ndege ndogo zenye kuwaunganisha watalii na idadi yao haijulikani.
Abainisha kuwa moja ya sababu za mafuriko hayo ya watalii wanaotua KIA ni filamu ya Royal Tour iliyozinduliwa na Rais Samia na kuoneshwa sehemu mbalimbali duniani juu ya vivutio vya utalii vilivyoko nchini.
“Kwa zaidi ya miaka miwili hali ilikuwa ngumu juu ya kuja kwa watalii na hiyo ilitokana na kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19 ulioenea sehemu mbalimbali duniani kabla ya kupatikana chanjo.
“Baada ya kupatikana chanjo ya Covid-19 na filamu ya Royal Tour kuzinduliwa, upepo umebadilika na wageni kuingia kwa wingi nchini tofauti na hiyo miaka miwili iliyopita,” amesema Mwakatobe.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Watoa Huduma za Utalii (TATO) Mkoa wa Arusha, Cyrili Ako amesema asilimia kubwa ya wageni wanaokuja nchini ni wale waliohamasishwa na filamu ya Royal Tour.
Ako amesema kuwa filamu hiyo imehamasisha kwa kiasi kikubwa watalii kuja kutalii nchini, na ndio maana kwa sasa kuna idadi kubwa ya wageni Arusha na sehemu nyingine za vivutio nchini kwa ujumla.
“Kama hali itakuwa hivyo kwa mwakani, nchi itafikia malengo ya kupokea wageni wengi zaidi tofauti na miaka ya nyuma na kuongeza pato kubwa la nchini na uchumi kukua zaidi,” amesema Ako.
Ikumbukwe kuwa Serikali kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeweka lengo la Tanzania kupokea watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025, ambao ni wa mwisho wa utekelezaji wa ilani hiyo.
Kutokana na idadi kubwa ya watalii mkoani Arusha, inaelezwa kuwa hata kampuni za utalii zimekumbwa na uhaba wa magari ya kuwapeleka watalii mbugani.
Mbali ya Arusha, Visiwa vya Zanzibar navyo kwa sasa vinapokea idadi kubwa ya watalii ambao wanatembelea maeneo ya vivutio visiwani.
‘Arusha imejaa watalii’, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter Julai 24, mwaka huu.
Akimjibu Zitto, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), Arafat Haji alisema ‘Zanzibar nayo imefurika watalii’.
Zitto na Haji wote wamezishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na ile ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuwekeza kwenye upanuzi wa miundombinu ikiwamo viwanja vya ndege na bandari, ili kukabiliana na ongezeko hilo la watalii.
Zitto amebashiri kuwa huenda Tanzania sasa ikaweka rekodi kwa kupata dola za Marekani bilioni tatu kwa mwaka huu kutoka kwenye utalii, sawa na Sh trilioni saba.
Mwaka jana, Tanzania ilipata dola za Marekani bilioni 1.4 kutoka kwenye sekta ya utalii.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema ndege ya Shirika la Ndege la KLM la Uholanzi usiku wa Agosti Mosi, mwaka huu ilishusha abiria zaidi ya 250 KIA.
“Kwa kweli kishindo ambacho Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekisababisha katika sekta ya utalii ni kikubwa sana,” aliandika Msigwa katika ukurasa wake wa Twitter.
Mbuga za wanyama na vivutio vikubwa vya watalii nchini zikiwamo Ngorongoro, Serengeti, Kilimanjaro, Arusha na Zanzibar, ni miongoni mwa maeneo ambayo kwa sasa watalii ni wengi.
“Kwa kweli hii haijawahi kutokea. Sijawahi kuona idadi kubwa ya watalii namna hii Arusha tangu nizaliwe. Rais Samia anastahili pongezi kwa kutuletea neema hii kupitia Royal Tour,” alisema dereva wa watalii jijini Arusha, Paul Mollel.