25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Jitihada za JPM zaongeza ulipaji kodi Tanga

Na MWANDISHI WETU -TANGA

WAFANYABIASHARA wa Mkoa wa Tanga wamesema hawaoni shida ya kulipa kodi baada ya kuona utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayofanywa na Rais Dk. John Magufuli kupitia kodi zao.

Wametoa kauli hiyo wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayofanywa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka Makao Makuu wakishirikiana na maofisa wa TRA Mkoa wa Tanga.

Maofisa hao waliwatembelea wafanyabiashara hao kwenye maduka yao jijini Tanga kwa lengo la kuwaelimisha na kuwakumbusha kulipa kodi kwa wakati.

Mfanyabishara wa ukwaju wa jumla na rejareja, Thabiti Salimu alisema kuwa atamshangaa mfanyabiashara anayekwepa kulipa kodi, hususani kipindi hiki ambacho wameona miradi mingi ikitekelezwa kupitia kodi zao.

“Rais Dk. Magufuli anatumia kodi zetu vizuri, tunaona utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo, hivyo lazima tuendelee kulipa kodi la sivyo kazi ya utekelezaji wa miradi hii itakwama,” alisema Salimu.

Alipongeza mpango ulioanzishwa na mamlaka hiyo wa kuwatembelea wafanyabiashara na kuwasikiliza, akisema ni mzuri ambao unapaswa uendelee kutokana na umuhimu wake kwa ustawi wa mlipakodi.

Kwa upande wake, Dina Mbenu alisema ikiwa wafanyabiashara watakwepa kulipa kodi, watasababisha madhara ya kiuchumi na kuathiri jitihada za Rais Magufuli kuboresha miundombinu ikiwemo barabara.

Dina alisema hatua ya maofisa wa TRA kuwatembelea kwenye maduka yao kwa lengo la kuwahamasisha kulipa kodi na kusikiliza kero na maoni yao, inawasaidia kutopoteza muda kwenye ofisi za mamlaka hiyo wakisubiri kuhudumiwa.

Naye Ofisa Msimamizi Mkuu wa Kodi, Julius Mjenga alisema zoezi la kuwatembelea wafanyabiashara ni endelevu na kabla ya kufanyika Tanga, limeshafanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Morogoro.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kutoa elimu ya kodi, kuwakumbusha wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati, kusikiliza maoni yao pamoja na changamoto kwa ajili ya kuzitatua.

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Specioza Owure, aliwaomba wafanyabiashara kuunga mkono zoezi linalofanywa na maafisa wao la utoaji elimu ya kodi, kusikiliza maoni na changamoto zao kwa kuwa linalenga kuboresha huduma kwa mlipakodi.

“Niwaombe wafanyabiashara wote mkiwaona maofisa wanatembelea msifunge maduka, wapokeeni na kuwapa ushirikiano kwa kuwa wanalenga kuwaelimisha na kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye biashara zenu ambazo kwa pamoja tunaweza kuzitafutia ufumbuzi,” alisema Owure.

Alisema kuwa maofisa hao wakiwa mkoani Tanga watafanya zoezi hilo hadi Juni 30, lengo ikiwa ni kuwafikia wafanyabiashara wengi mkoani hapa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles