24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Jinsi ya kumfanya mtoto kuwa na nidhamu

children

KATIKA umri wa miaka miwili na mitatu, mtoto huwa tayari anatembea na hivyo huhitaji kujisikia huru. Ndio umri anaojifunza kuongea na hivyo hujaribu kufanya mengi kuona anayoweza kuyafanya bila msaada.

Hata hivyo, katika umri huu mtoto bado hajawa na uwezo wa kufikiri matokeo anayoyafanya na hana uwezo wa kuwaza wengine wanafikiria nini. Kwa hiyo, bila tahadhari, mtoto huweza kuanza kujifunza tabia zisizotarajiwa. Ili kumfanya awe tayari kufanya yale anayoelekezwa bila kushindana sambamba na kuwa na kiasi katika mambo yake, tunashauriwa kufanya mambo kadhaa.

Kutabirika kwa matarajio

Tunashauriwa kujenga mazingira yanayoeleweka kwa mtoto ili kumfanya ajue tunatarajia nini kwake. Mazingira hayo ni pamoja na kuweka mpangilio wa mambo yasibadilika kwa siku kama vile wakati gani anapaswa kuwa amelala, wakati wa kuamka, kula, kucheza na kadhalika. Kutokubadilika kwa mambo haya ya kawaida ya kila siku humfanya mtoto aelewe kinachotarajiwa kwake na hivyo huwa rahisi kuwa na nidhamu.

Kadhalika,  ni vyema mtoto aweze kutabiri matokeo ya makosa yake. Kwa mfano, anapoadhibiwa kwa kijitabia fulani kisichofaa, ni vizuri aendelee kuadhibiwa na wakati mwingine atakaporudia kosa kama hilo. Lengo ni kumjengea uwezo wa kutabiri matokeo ya atakachokifanya baadae.

Kusikiliza na kuwaelewa

Mtoto wa umri huu hana uwezo wa kufikiri kwa kina kama mtu mzima. Tunao wajibu wa kujishusha kiuelewa ili kuelewa ‘dunia yake’. Kujisikia kueleweka kunamfanya awe mwepesi kutii na kusikiliza.

Vile vile, kumfanya aamini hisia na maoni yake yanaheshimiwa kunamwongezea ari ya kuwa na nidhamu. Mathalani, kumwuliza nguo anayopenda kuvaa baada ya kuoga humfanya ajisikie anathaminika na huongeza uwezekano wa kuwa msikivu hata katika mazingira mengine.

Kumsahaulisha hasira zake

Mtoto kama mtu mwingine yeyote hupatwa na hasira pengine kwa kuhisi haeleweki. Hasira zinaweza kufanya afanye asichotarajia. Katika mazingira haya ya hasira, kujaribu kumgeuza lengo kunaweza kuwa suluhu kuliko kumwadhibu akiwa na hasira.

Kwa mfano, anapokasirika kwa kunyimwa kuchezea kifaa cha hatari anachokitaka, ni rahisi kumaliza matatizo kwa kumwonesha kingine tunachojua kinamvutia. Kufanya hivyo ni kumsahaulisha kwa kujua kuwa katika umri huu mdogo, mtoto kwa kawaida hana uwezo wa kuzingatia kitu kwa muda mrefu.

Kutoshinda naye

Kutoa adhabu kwa hasira bila kujali hisia za mtoto kunaweza kutafsirika kama kushindana naye. Pamoja na umuhimu wa kumwajibisha mtoto kwa makosa yake, wakati mwingine adhabu si njia pekee. Kupuuza tabia husika yaweza kuwa dawa mbadala na yenye ufanisi sawa na hata zaidi ya adhabu.

Upo ukweli kuwa tunapomzoesha mtoto adhabu zinazoumiza mwili tunamwonesha mfano mbaya kwa kufunza tabia ya kutumia nguvu katika kutatua migogoro yake. Kufumba macho na mara moja moja kumwacha apate anachotaka kunaweza kusaidia kumfanya akubaliane na matakwa baadae bila upinzani.

Kwa hakika kujenga nidhamu ya mtoto wa umri huu haiwezi kuwa kazi nyepesi hata kidogo. Kuna mchanganyiko wa matarajio ya mtoto anayetamani kujua anachoweza kufanya na mzazi mwenye shauku ya kuona mtoto anajifunza nidhamu. Uwiano wa mawili hayo ni changamoto kubwa inayodai uvumilivu wa hali ya juu. Tunahitaji uvumilivu huo ili kuwafundisha watoto wetu kuwa na tabia njema kadri wanavyokuwa kimwili na kiakili.

 

Mwandishi ni mwalimu wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Anapatikana kwa [email protected], 0754 870 815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles