25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jinsi ya kuikuza, kuiendeleza mbegu ya uongozi iliyoko ndani yako – 2

NA DK. CHRIS MAUKI

KILA mmoja wetu amebeba mbegu ya uongozi ndani yake, tunapoikuza kwa hekima mbegu hii inaanza kuonyesha matunda dhahiri. Mbegu ya uongozi inapowezeshwa, matokeo yake huwa makubwa katika maendeleo ya jamii ndogo hadi taifa kwa ujumla.  

Huwezi kuwa na taifa lililoendelea pasipo kuwa na  watu walioendelea na walioendelezwa katika mbegu zao za kiuongozi ndani yao, si serikali iliyo na nguvu inayosababisha  nchi iliyo na nguvu na uwezo bali ni watu waliiowezeshwa (wenye nguvu na uwezo) wanaotengeneza taifa lililo kuu.  

Sote tuna wito wa uongozi katika maisha yetu, na huo uongozi unathibitishwa kwa yale majukumu ya usimamizi.  Kwa hiyo majukumu yasipoelezwa wazi inamaana uongozi wako hauwezi kukamilika .  Na uongozi tunaweza kuelezea kwa kuangalia majukumu yaliyotekelezwa.  Kamwe huwezi kuwa kiongozi wa mwanasheria kama   wewe si mwanasheria.  Watu wengi wangependa kuwa viongozi pasipo kujulikana ni nini majukumu yao (majukumu haya ndiyo yatakayo thibitisha uongozi wako)  

 Uongozi pia huthibitika pale tunapoweza kuelezea eneo letu la kazi, maeneo yetu ya kiutendaji yanapojulikana wazi basi hata uongozi wetu unakuwa na mguso kwa wahusika. Suala zima la uongozi ni kuhusu kujisimamia wewe mwenyewe, (self management) kusimamia majukumu uliyopewa, (management of responsibilities), kusimamia mali vitu vilivyopo katika himaya yako ya uongozi, (management of materials) na kusimamia rasilimali watu uliyopewa, (management of human resources) 

Tuna viongozi wengi wabovu duniani maana hawawezi kusimamia vile walivyovipewa. Daima ni wasimamizi walio wazuri peke yao watakaoweza kuwa viongozi bora usimamizi binafsi huanzia  na sisi wenyewe, je unaiweza nyumba yako. Jiulize, jeutawezaje kuwatawala wengine kama wewe mwenyewe umejishindwa?

Huwezi ukajisimamia vema wewe mwenyewe kama huwezi kusimamia  muda wako vizuri. (Self management is actually time management).  Kila habari ya mafanikio makubwa ya mtu unayoisikia, nyuma yake ukiifuatilia utakuta mtu aliyetunza na kuukomboa wakati wake vema.  Kiujumla Waafrika ni wabovu sana katika kuukomboa na kuutumia muda.  Mtu anaweza kukaa na mtu mwingine kwa saa matatu pasipo lolole la maana linaloendelea.  Mtu anaweza kuipoteza siku nzima pasipo kufanya chochote na hii ndiyo maana ya umasikini wetu. Tunaposema neno “life time” (muda wa maisha) tunamaanisha hatuwezi kuvitenganisha muda na maisha, maana yake nyingine ni kwamba kama huwezi kuutunza muda basi huyawezi maisha.

Usipoweza kusimamia muda wako vema unapoteza sehemu muhimu sana maishani mwako, na unajiweka katika hatari ya vishawishi vingi. Wanasema nafsi isiyo na kitu cha kufanya wala kuwaza ndiyo karakana ya ibililsi. (An idle brain is the workshop of the devil)

Usitumie muda wako tu kwa maana ya kuutumia, bali wekeza katika muda wako. Hapa namaanisha kuwa yale tunayoyafanya katika kuujali muda wetu yafanyike faida katika siku za usoni.  Wakati ni kitu au rasilimali ambayo  wote tumepewa sawa sawa, wote tuna saa 24, lakini wachache wetu hutumia kwa kuwekeza, na kinyume chake wengi wetu huruhusu  saa hazo kupita pasipo wala kuhisi kuwa tunapoteza kitu cha muhimu.  Wengi husema hawana muda ingawa bado wanapata muda wa baadhi ya vitu kama vile kula, kulala, kuongea, kuangalia sinema nk.

Usimamizi wa jukumu 

Jukumu lako lisipowekwa wazi na kueleweka uongozi wako hauwezi kueleweka. Kila kiongozi mkuu aliyewahi kutokea katika historia amekuwa na majukumu halisi yaliyoelezwa kwa ajili yake na umuhimu wa viongozi hao ulikuwa katika uwezo wao wa kusimamia majukumu hayo.

Mara nyingi ni ngumu kusimamia au kuongoza ukiwa mwenyewe na kwahiyo yalazimu kuweka mfumo wa usimamizi ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa. 

ofisi, kampuni au huduma yeyote inayoongozwa na mtu mmoja pekee lazima itakuwa na shida.

Usimamizi wa jukumu unahusiana sana na ujuzi. Ujuzi hauji tu, bali unatafutwa,  ujuzi haurithishwi bali hutafutwa kwa kujifunza.  Ujuzi ulionao ndiyo unaelezea ubora wa usimamizi wako. Unahitaji muda wa kutosha ili uweze kutafiti na kujifunza ili kujenga uwezo wa usimamizi wako. Je; unajua nini na una ujuzi gani katika kile unachokifanya au unachotamani kukifanya? Kumbuka kuwa, kazi kubwa hufanywa kwa ujuzi mkubwa na kazi ndogo hufanywa kwa ujuzi mdogo.  Kamwe huwezi kusimamia kitu usichokuwa na ujuzi nacho. Pia,  kamwe hauhitaji kuwa mkuu ili uweze kusimamia vema bali unahitaji kusimamia vema ili uwe mkuu. Ni usimamizi mzuri peke yake unaokuza kiwanda, ofisi, kampuni, huduma na hata taifa.

Kama nilivyokwisha kusema awali, watu wengi wa jamii yetu ni wabovu sana katika kusimamia muda na kwahivyo hawawezi kusimamia majukumu yao iwapasavyo. Kama wewe si msimamizi mzuri basi lazima utakuwa mfujaji mzuri, na ukweli ni kwamba rasilimali zisizosimamiwa vyema huharibiwa  vyema. 

Hii ndiyo sababu tunakuwa na ombaomba wengi katika nchi yetu kutokea ngazi za chini hadi za juu. Mataifa mengi ya Afrika ni ombaomba wazuri kwa mataifa madogo ya ulaya ambayo hayana hata rasilimali yoyote ukilinganisha na rasilimali walizonazo Waafrika, tofauti ni kwamba wao wana tumia na kusimamia vema rasilimali kidogo waliyo nayo, wakati sisi tunafuja vile tulivyonavyo. Wakati wote huwezi kuwa mfujaji bila ya kuwa mhitaji mkubwa. Jiulize, je unatumiaje muda wako, unawekeza au kuufuja?

Kwa kawaida kama hakuna bajeti (mchanganuo wa mapato na matumizi) ambayo una wajibika kwayo basi ufujaji haukwepeki kamwe. Kizazi kisichoishi kwa bajeti ni kizazi potovu na fujaji, ndiyo wale wanaopeleka watoto wao katika shule wasizoweza kuzilipia, ndiyo wale pia wanaonunua vitu visivyo lazima sana  kwa muda fulani ili mradi tu na wao waonekane wanavyo.

Ukisimamia vema bajeti ya familia yako kamwe hautakuwa mwombaji. Usimamizi mzuri wa rasilimali fedha ni mlango wa kuingia kwenye kupanuka, kuongezeka au kufanikiwa. Kila kinachoongezeka kinaongezeka kwa maana kimesimamiwa vema. Unapoanza kufuja rasilimali ulizonazo unaufunga mustakabali wako, unaifunga milango yako yote ya kufanikiwa. Jifunze kusimamia vema rasilimali watu,        (watu wanaokuzunguka) fahamu kwamba kamwe huwezi kufanikiwa wewe mwenyewe, lazima uwe na watu unaowategemea, watu hao lazima wawe na usimamizi mzuri. Zipo nyakati utahitaji kuwavumilia, zipo nyakati utahitaji kuwasamehe, zipo nyakati utahitaji kuwapongeza na zipo nyakati utahitaji kuwa mkali na hata kuwafukuza pale inapobidi kwa maana katika nyakati kama hizo usipowafukuza wao, watakufukuza wewe. Kuna kanuni ya usimamizi inayosema usimwajiri mtu yeyote ambaye hutoweza kumfukuza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles