JINSI TIMU LIPUMBA ILIVYOLAMBA MIL. 300/-

1
721
Profesa Ibrahim Lipumba
Profesa Ibrahim Lipumba
Profesa Ibrahim Lipumba

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

UPANDE wa uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), chini ya Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, unadaiwa kulamba Sh milioni 369.378 za ruzuku kinyume cha utaratibu.

Inadaiwa kuwa fedha hizo zimetolewa ndani ya siku moja katika matawi matatu tofauti ya Benki ya NMB kwa kutumia akaunti ya chama na baadaye kuhamishiwa kwa mtu binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF ambaye hatambuliwi na Msajili, Julius Mtatiro, alisema fedha hizo zilitolewa kutoka Hazina na kupelekwa NMB tawi la Temeke.

Wakati Mtatiro akidai hayo, Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa CUF, Abdul Kambaya, alidai fedha hizo zimetolewa kihalali kama walivyofanya upande wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ambao alidai walitoa Sh milioni 80 kupitia Benki ya NBC.

Pamoja na hali hiyo, Mtatiro alisema fedha hizo ziliingizwa katika akaunti binafsi ya mtu aliyetambulika katika muamala kwa jina la Mhina Masoud Omary.

Alisema kwa niaba ya Baraza Kuu la Uongozi la CUF ambalo limemteua yeye kuongoza, hana budi kuwajulisha wanachama kuwa CUF imeibiwa fedha hizo za ruzuku ambazo alidai zimetoroshwa na watu wasiojulikana.

“Fedha hizo zilitoroshwa kutoka Hazina ya Serikali Kuu Januari 5 na kuingizwa kwenye Akaunti ya NMB Tawi la Temeke yenye jina la The Civic United Front ikiwa na akaunti namba 2072300456.

“Bodi ya Wadhamini ya CUF ambayo ndiyo msimamizi wa jumla wa masuala ya akaunti za fedha na mali za chama hicho, haijatambua akaunti hiyo na haikuwahi kuidhinisha ipokee ruzuku ya CUF kutoka Serikali Kuu,” alisema Mtatiro.

Alisema Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif, ndiye muwajibikaji mkuu wa masuala ya fedha na mali za chama, hivyo haitambui akaunti hiyo na hajawahi kumwandikia Msajili wa Vyama vya Siasa kumpa akaunti hiyo ili iwekewe fedha za ruzuku ya CUF.

Mtatiro aliongeza kuwa vikao vya kitaifa vya chama hicho, kwa maana ya Kamati ya Utendaji ya Taifa iliyokutana hivi karibuni kumpitisha mgombea ubunge Jimbo la Dimani, Zanzibar na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, havikuwahi kupitisha uamuzi wowote kwamba fedha za CUF ziwekwe katika akaunti hiyo.

“Baada ya kugundua utoroshwaji huo wa fedha za ruzuku ya CUF ambazo ni fedha za umma na zina masharti na taratibu zake katika kutolewa, tumejiridhisha kuwa akaunti ambayo Hazina ya Serikali Kuu wameshiriki kuitumia kutorosha fedha za umma na mali ya CUF, ni akaunti ya CUF ambayo hutumiwa na Wilaya ya Temeke kwa ajili ya kupokea mgawo wa ruzuku kutoka kwa chama Taifa.

“CUF kinazo akaunti katika kila wilaya ya kichama, kwa mfano Wilaya ya Kinondoni ya CUF wanayo akaunti ya benki ambayo wanaitumia kupokea fedha zilizoidhinishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ya Chama kwa mujibu wa Katiba, Wilaya ya Ilala pia ina akaunti ya namna hiyo, Mtwara  na wilaya nyinginezo,’’ alisema Mtatiro.

Aliongeza kuwa baada ya watu wanaomsaidia aliyemtaja kwa jina la  ‘Bwana Yule’ kuivuruga CUF na kuona kuwa Bodi ya Wadhamini  imezuia njama za ufunguaji wa akaunti mpya ya CUF Ilala, wakatumia mbinu ya namna ile ile kwa njia tofauti kwa Temeke.

Mwanasiasa huyo aliendelea kueleza jinsi fedha hizo zilivyotoroshwa, kuwa siku mbili kabla ya utoroshaji huo, ulisukwa mpango wa kuwaondoa baadhi ya viongozi wa CUF wa Wilaya ya Temeke kwenye utiaji saini unaoihusu akaunti tajwa.

Alisema uondoaji huo ulikwenda sambamba na kuwageuza baadhi ya wateule wa Profesa Lipumba wanaofanya kazi za kukihujumu chama kutokea Buguruni.

Mtatiro alisema watia saini wapya walioshiriki ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara ambaye ni Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya na mtu mwingine aitwaye Thomas Malima, ambao wote wapo kwenye mgogoro na chama hicho wakipinga kusimamishwa uanachama wao.

“Yaani ni kama vile leo hii ruzuku ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) itoroshwe na kuwekwa kwenye akaunti ya NMB ya CCM ngazi ya wilaya huko Kahama. Kisha fedha hizo ziondolewe kwenye akaunti hiyo ya wilaya na kuingia kwenye akaunti ya mwana CCM aliyesimamishwa uanachama na halafu mwana CCM huyo azitoe fedha hizo na kuzipeleka kusikojulikana, hali ingekuwaje?” alisema na kuhoji Mtatiro.

FEDHA ZILIVYOINGIZWA

Alisema siku moja baada ya NMB na wala njama hao kukamilisha mchakato wa kubadilisha watia saini wa akaunti ya CUF inayomilikiwa na Wilaya ya Temeke, Januari 5 ndipo Hazina ikaweka fedha hizo bila kuchelewa.

Mtatiro alisema Hazina walipotorosha fedha hizo, watia saini wapya wa Akaunti ya NMB ya Wilaya ya Temeke waliulizia kiasi cha fedha kilichomo kwenye akaunti hiyo na walifanya hivyo katika tawi la NMB Mandela Road.

Alisema siku ya pili yake yaani Januari 6, aliowaita watia saini wakiongozwa na Malima walikwenda katika Benki ya NMB Tawi la Temeke na kufanya mambo mawili, moja ikiwa ni kuhamisha Sh milioni 69, kisha wakahamisha Sh milioni 300 kwenda kwenye akaunti ya mtu binafsi.

“Mchezo wote huo umefanyika ‘chapchap’ kama zilivyochotwa pesa za Escrow,” alisema.

Akiendelea kueleza, Mtatiro alisema kuwa akaunti ya mtu binafsi iliyotumika kutoroshea fedha hizo kutoka kwenye akaunti ya Wilaya ya Temeke, ni ya NMB yenye namba 41401600207 inayomilikiwa na Mhina ambaye ni Diwani wa CUF wilayani Handeni na kwamba wameeleza kuwa ni mtu wa karibu wa Profesa Lipumba.

Alisema wakati fedha hizo zinahamishiwa kwenye akaunti ya Mhina haikukutwa na senti tano.

“Na hii ni mara ya kwanza tunashuhudia kuwa fedha za chama zilizotoroshewa kwenye akaunti ya ngazi ya wilaya zinaondolewa haraka na kuwekwa kwenye akaunti ya mtu binafsi,’’ alisema Mtatiro kwa mshangao.

Aliendelea kueleza kuwa Januari 9, mwaka huu, akaunti ya Mhina ilikuwa kwenye mchakato mkubwa wa kuondoa fedha hizo kutoka kwenye akaunti hiyo.

FEDHA ZILIVYOONDOLEWA

Mtatiro akiendelea kuelezea mlolongo wa uondoaji wa fedha kutoka akaunti ya Mhina, alisema alianza kazi ya kuondoa fedha hizo majira ya asubuhi Januari 6, mwaka huu kwa kuanza kuondoa Sh milioni 100 tawi la Magomeni.

“Kisha akiwa hapo hapo Magomeni akatoa tena Sh milioni 50 halafu akaelekea tawi la Kariakoo na kutoa Sh milioni 100 na mwisho akiwa hapo hapo Kariakoo NMB akatoa tena Sh milioni 49.5.

“Wakati Mhina anazunguka kwenye matawi haya kutoa fedha hizi, jana alipewa ulinzi wa Jeshi la Polisi waliokuwa wamevalia kiraia wakiwa kwenye magari ya CUF na aliambatana na Thomas Malima wakiwa chini ya usimamizi wa watu wengine wawili, Magdalena Sakaya na Abdul Kambaya.

“Baada ya kutorosha fedha hizo zote, akaunti ya Masoud Mhina imebakia na Sh 207,907 kama zawadi maana wakati inawekewa Sh milioni 300 haikuwa na hata senti tano,” alisema.

Mtatiro alisema kuwa Oktoba 10 mwaka jana, Msajili wa Vyama vya Siasa alimwandikia Mwenyekiti na Katibu  wa CUF na kuwajulisha kwamba ofisi yake inasitisha ruzuku ya CUF kwa kile alichokiita fedha hizo ni za umma ambazo zinahitaji usimamizi mzuri katika matumizi yake.

“Kwa kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ina dhamana ya kugawa fedha za ruzuku kwa vyama vya siasa vinavyostahili na kusimamia uwajibikaji katika matumizi ya fedha hizo, hivyo baada ya tafakuri ya kina aliona ni busara kwanza kusimamisha kwa muda mgawo wa ruzuku.

“Katika maandiko kwa vyama, barua ya Msajili ilikuwa na namba yenye Kumb. Namba HA.322/362/14/17,” alisema.

Alisema CUF inafahamu tangu Msajili aiandikie barua kusitisha ruzuku ya chama hicho, sasa ni miezi mitano ambapo CUF inadai ruzuku ya Sh milioni 635.

Chama hicho pia kinamwomba Rais Dk. John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Gavana wa Benki Kuu (BOT), Takukuru, Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali na vyombo vingine vinavyohusika, kuchukua hatua za dharura za kuokoa fedha hizo za umma.

Kutokana na yote hayo, Bodi ya Wadhamini ya CUF tayari inakutana na Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa kile alichokiita shambulio kuelekeza hatua za kiutawala na kisheria za kuchukua haraka.

 HAZINA WAJIBU

Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ben Mwaipaja, alikiri Hazina kutoa kiasi cha Sh bilioni 7.16  Julai hadi Novemba mwaka jana.

“Sisi kama wizara tuna jukumu la kupeleka fedha hizo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na si kupeleka moja kwa moja kwenye vyama, Msajili yeye ndiye anayejua mgawanyo wake, hivyo hatuhusiki kwa hilo,’’ alisema Mwaipaja.

 KAMBI YA LIPUMBA

Wakati hayo yakiendelea, Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, Kambaya, alisema hawana sababu ya kumjibu Mtatiro na genge lake, bali kwa kuwa kumeibuliwa hoja inayohusu viongozi halali, wanaona umuhimu wa kutoa ufafanuzi.

Alisema CUF inaongozwa na utaratibu wake ikiwamo Katiba, na kama anaona ni kiongozi wa kitaifa, ni vema awasilishe malalamiko yake katika vikao vya chama badala ya kulalamika kwenye vyombo vya habari.

“Katibu Mkuu wa chama hiki ni Maalim Seif Sharif Hamad na Mwenyekiti ni Profesa Ibrahim Haruna Lipumba. Ni kweli CUF tumeomba fedha zetu za ruzuku ili ziweze kutusaidia kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 20 kwa upande wa Tanzania Bara.

“Ni vyema Watanzania wakafahamu kwamba kupitia kwa Shaweji Mketo, upande wa Maalim Seif Sharif Hamad umetamka bayana kwamba haujasimamisha mgombea kwenye kata yoyote katika uchaguzi huu mdogo unaotarajiwa kufanyika Januari 22, mwaka huu.

“Kwa upande wa Bara, CUF tumesimamisha wagombea kwenye kata 14 kati ya 20 zinazopaswa kurudia uchaguzi.  CUF ni chama cha wananchi, hatuwezi kuacha kusimamisha wagombea na kuamua kuunga mkono wagombea wa Chadema kama ilivyoelekezwa na Katibu Mkuu kupitia Shaweji Mketo,’’ alisema Kambaya.

Alikiri kutolewa kwa fedha hizo ambazo ziliingizwa kwenye akaunti ya chama ambazo sasa zinatumika kwenye shughuli ya uchaguzi wa marudio.

“Mbona sisi hatujatoka mbele ya umma na kulalama hatua ya Maalim Seif Sharif Hamad na wale wanaojiita genge mbona si wa kweli, waeleze basi Oktoba mwaka jana walivyotoa Sh milioni 86 kupitia Benki ya NBC bila kuhusisha upande kupitia Naibu Katibu Mkuu Bara Magdalena Sakaya ambaye ni mmoja wa watia saini kwenye akaunti hiyo.

“Sisi hatukuona shida pamoja na kutojulishwa kwa kuwa tunajua kuwa fedha zimekwenda kwenye Uchaguzi wa Jimbo la Dimani. Mtatiro hawezi kuyafahamu haya kwa kuwa si kiongozi wa chama hiki,’’ alisema Kambaya huku akiwataka wana CUF kupuuza kelele hizo.

1 COMMENT

  1. Katika mambo ya aibu na ambayo yatataligharimu taifa nasi Watanzania kwa jumla ni pale tunapopuuza mambo ambayo baafi ya wanazi wa kisiasa wanadhani yana Tina upande wao. Inawezekana wanufaika wanatazama faida inayopatikana Leo na si hasara itakayofuata baadae. Ikiwa ufisadi unapigwa vita huku viashilia vya kukumbatia dalili za ufisadi zikionekana basi tuna safari ngumu huko mbele. Kwani hatutofautiani na mtu anaesafisha sakafu huku akiingiza matope. Mungu Ibariki Tanzania

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here