33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JINSI MBOWE ALIVYOPEKULIWA NA POLISI

Na Mwandishi wetu – dar es salaam


NI kama sinema. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na namna vyombo vya usalama vilivyotumia zaidi ya saa nane kupekua nyumba mbili za Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, anayetuhumiwa kuhusika na dawa za kulevya.

 Mbali na mambo mengine, sinema hiyo inakolezwa na namna Mbowe alivyokamatwa na askari hao eneo la darajani, Kawe wakati akielekea Kituo Kikuu cha Polisi (central) Dar es Salaam, na kumuhoji kwa takribani saa tano kabla ya kurudi nyumbani kwake Kawe kwa upekuzi.

Wakili wa Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Frederick Kihwelo, aliliambia MTANZANIA jana kuwa mteja wake alihojiwa kituoni na jopo la takribani watu 20, wakiwamo maofisa wa polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Usalama wa Taifa na Uhamiaji.

Kihwelo aliyekuwa ameambatana na Mbowe tangu kituo cha polisi hadi nyumbani kwake wakati upekuzi ukifanyika, alisema mteja wake huyo aliyekamatwa juzi saa 9:02 alasiri, akafikishwa Kituo Kikuu cha Polisi saa 9:10 na kuondolewa saa 11:40, alisema baada ya upekuzi huo, walijiridhisha kwamba hakutafutwa kwa sababu ya dawa za kulevya bali ni kujua masuala ya chama na taarifa zake za fedha.

 

UPEKUZI ULIVYOFANYIKA

Kihwelo aliliambia MTANZANIA kwamba walivyokuwa wanatoka Kituo Kikuu cha Polisi, walikatazwa kuondoka na gari la Mbowe ambalo alikuwa akilitumia awali kabla ya kushushwa na kupakiwa katika gari la polisi.

Alisema kuwa polisi waliwataka kuacha gari hilo kituoni hapo kwa sababu litafanyiwa pia upekuzi baada ya ule wa nyumbani kukamilika.

“Lile gari lilikuwa limeambatana na lililomchukua pale Kawe hadi Central, wakati tunataka kwenda nyumbani kwa ajili ya upekuzi, wakatuambia tuliache na kisishushwe kitu chochote, kwa hiyo dereva akaliacha na kulifunga kisha tukaelekea nyumbani,” alisema Kihwelo.

Alisema kwa kuwa hawakukaa kwenye foleni, walitumia muda mchache kutoka katikati ya mji hadi Kawe nyumbani kwa mwenyekiti huyo.

Pamoja na kuwahi huko, walikwama kuanza kufanya upekuzi baada ya kukuta msichana wa ndani hayupo.

“Tulipouliza majirani tukaambiwa amechukuliwa na polisi na kupelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay, ikabidi wale polisi waende wakamchukue ili atufungulie mlango na kisha wakamwachia. Sasa hapa unapata swali jingine tena, kama walikuwa wanafuatilia taarifa za dawa huyu dada walimchukua kwa ajili gani?” alisema Kihwelo. 

Alisema kuwa mlango ulipofunguliwa, kukatokea tena ubishani baada ya kutaka kuwakagua askari hao kabla ya kuingia ndani kuanza upekuzi wao.

“Tuliwaambia tutajuaje kama wana vitu wanataka kuja kuweka, kisha waseme wamevikuta ndani, lakini baadaye wakasema wao wana nia nzuri tu na wala hawana lengo baya, ikabidi sasa tuseme waingie angalau watano kwa sababu pale walikuwa zaidi ya 10,” alisema.

Alisema walikagua nyumba hiyo kuanzia majira ya saa 12 jioni hadi saa 3:15 usiku na kwamba vitu walivyoondoka navyo kwenye nyumba hiyo ni kadi tatu za magari – mawili yakiwa ni ya kubebea wagonjwa na moja la Mbowe, kadi mbili za benki, kitabu alichokuwa akitumia kuandika taarifa wakati wa vikao (diary) na kifaa cha kielektroniki cha kuhifadhia taarifa (external disc) ambacho kilikuwa kipya na hakijaanza kutumika.

Kihwelo alisema baada ya kutoka kwenye nyumba hiyo ya Kawe, walielekea kwenye nyumba nyingine iliyopo Mikocheni, ambako upekuzi pia ulifanyika hadi saa sita usiku.

Alisema katika nyumba hiyo, waliondoka na nyaraka za chama ikiwa ni pamoja na za kikundi cha ulinzi (Red Brigade) na baadhi ya taarifa za Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa chama hicho (Chaso).

“Kati ya jambo lililonishangaza, hawa jamaa walivyokuwa wakiona nyaraka ya chama wanafurahi kweli, sasa unajiuliza kama kweli suala hapa ni dawa za kulevya, mbona wanafurahia hivi kupata nyaraka za chama?” alisema Kihwelo.

Alisema askari hao ambao walikuwa katika gari mbili,  moja aina ya Nissan Patrol na jingine Toyota Land Cruiser hardtop, baada ya kuridhika na upekuzi huo waliondoka tena na mteja wao kuelekea kituo kikuu cha polisi ambapo walifanya shughuli hiyo tena kwenye gari la mbunge huyo.

Baada ya upekuzi huo, alisema saa saba ndipo walipowaruhusu kwa masharti ya kuripoti tena leo.

“Lakini baada ya hukumu ya leo (jana), ndiyo hatuendi tena polisi hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa,” alisema.

Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni jana, Jeshi la Polisi lilikuwa halijatoa taarifa rasmi ya vitu walivyochukua katika upekuzi huo.

Februari 8, mwaka huu baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutangaza jina la Mbowe kuwa ni mmoja wa watu wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya na kumtaka afike polisi kuhojiwa, malumbano makali yaliibuka bungeni juu ya askari kukamata ovyo wabunge.

Siku hiyo, wabunge wa upinzani walisusia kikao cha jioni baada ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, kukataa hoja ya wabunge hao waliotaka mhimili huo utoe tamko juu ya kamata kamata ya wabunge bila kufuata utaratibu.

Februari 10, Mbowe, akiwa mjini Dodoma aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kukana kuhusika kwa namna yoyote na biashara ya dawa za kulevya ama kuzitumia.

Februari 18, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alitoa saa 48 Mbowe kujisalimisha mwenyewe vinginevyo watamtafuta kwa njia wanazojua wao.

Wakati Spika wa Bunge, Job Ndugai, akihitimisha mkutano wa sita wa Bunge, alisema kama kuna kiongozi yeyote wa Serikali anamuhitaji mbunge, anapaswa kutoa taarifa kwake kwanza badala ya kutumia ubabe.

Ndugai aliwatoa hofu wabunge kuhusu hadhi ya Bunge na kusema kuwa hadhi ya chombo hicho haijashuka na kwamba mhimili huo hauna mgogoro wowote na Serikali wala mahakama.

Tangu alipotoa tamko hilo, mara kadhaa vyombo vya habari na waandishi wake wamekuwa wakifuatilia Bunge kama limepata ombi au taarifa kutoka polisi juu ya kumkamata Mbowe, na mara zote limekuwa likisema halijapokea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles