30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JINSI MAULID KITENGE ALIVYOMNUSURU NAPE NA BASTOLA

NA MWANDISHI WETU

MWANDISHI wa habari, Maulid Kitenge,  ambaye juzi alimnusuru aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye dhidi ya mtu aliyemshikia bastola wakati akielekea kuzungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Protea, jijini Dar es Salaam, amefunguka na kueleza kile kilichomsukuma aingilie kati.

Juzi, mara baada ya Nape kuwasili karibu na hoteli hiyo, ambayo inapakana na Kanisa la Mtakatifu Petro, lililoko eneo la Oysterbay, aliposhuka tu ghafla kijana huyo mrefu mweusi akiwa amevalia suruali ya jinzi, shati la mikono mirefu la mistari mistari pamoja na kofia, alimkimbilia na kumshika mkono kiongozi huyo akimtaka arudi kwenye gari.

Nape hakukubaliana na hatua hiyo, ambaye alimtaka kijana huyo aonyeshe kitambulisho, lakini hakufanya hivyo, zaidi alirudi hatua chache nyuma na kisha kutoa bastola iliyokuwa kiunoni kwake na kumtishia.

Wakati tukio hilo likitokea, ghafla alitokea kijana mwingine aliyekuwa amevalia suruali na fulana nyeusi akimsaidia yule aliyekuwa ameshika bastola kumsukuma Nape, ili arudi kwenye gari lake.

Ni katika mazingira kama hayo, ndipo waandishi wa habari waliokuwa ndani ya Hoteli ya Protea wakimsubiri Nape walipoanza kusogea, huku Mwandishi wa habari mashuhuri wa michezo nchini, Kitenge, akiwahi kufika na kwenda moja kwa moja katika eneo ambalo Nape alikuwa akisukumwa aingie ndani ya gari lake.

Kitenge alimsihi kijana huyo aache kumsukuma Nape na alipoonekana kubisha aliamua kumsukuma pembeni.

MTANZANIA Jumamosi jana lilizungumza na Kitenge, ambaye alisema:

“Niliona mtu anamtolea Nape bastola nikashangaa, kwani muda mfupi uliopita alikuwa waziri na isitoshe ni mbunge, sasa yule mtu aliambiwa ajitambulishe, lakini hakujitambulisha,” alisema.

Alisema tukio lile lilimshtua, kwani mtu huyo aliyekuwa ameshika bastola alikuwa akitetemeka sana, huku jasho likimtoka.

“Hatukumwelewa, kwanza hakutoa kitambulisho,” alisema Kitenge, ambaye juzi wakati akimwokoa Nape alisikika akimwambia kijana huyo aliyeshika bastola; “unaharibu bwana mwache, mwache bwana….”

Wakati tukio hilo linatokea walikuwapo waandishi wa habari wachache, huku wengi wao wakiwa ndani ya hoteli hiyo wakimsubiri Nape, lakini purukushani hizo ambazo ziliambatana na kelele ziliwashtua na hivyo kulazimika kukimbia kuelekea eneo la tukio.

Waandishi wa habari walivyofika wengi mtu huyo hakuweza kuonekana tena na ndipo Nape alifanikiwa kuzungumza nao.

Tukio hilo la kutolewa bastola lilitanguliwa na lile la Meneja wa Hoteli ya Protea, aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Suleiman, kutangaza kuzuia mkutano wake na waandishi wa habari usifanyike katika hoteli hiyo, kwa kile alichodai kuwa, ni maelekezo kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Susan Kaganda.

KITENGE GUMZO

Kutokana na kitendo hicho, mwanahabari huyo sasa amegeuka gumzo katika maeneo mbalimbali, hususan katika mitandao ya kijamii.

Andiko ambalo linasambaa sana kwenye mitandao ya kijamii, lakini halijulikani aliyeandika, ni lile lililoambatana na picha yake inayomwonyesha akikimbia huku likisomeka;

“Wanaume wa Dar walikuwa wanadharaulika sana, Kitenge kawaokoa…”

Si hilo tu, baadhi ya watu wamekwenda mbali na hata kuanza kuhoji nguvu alizonazo mwanahabari huyo kiasi cha kuweza kuhimili kumwondoa mtu huyo aliyeshika bastola.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles