Na Hadija Omary, Lindi
Ini ni kiungo muhimu sana ndani ya mwili wa mwanadamu, hufanya kazi zaidi ya 500 ambapo moja ya kazi ya yake ni kuchuja na kuondoa sumu kwenye damu.
Kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo matumizi ya pombe kupita kiasi, kunaweza kuleta shida katika ini na kusababisha ugonjwa wa sumu kwenye damu homa ya Ini ‘Hepatitis B (HBV).
Wataalamu wanaeleza kuwa moja ya njia za usambaaji wa homa ya ini ni kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambapo mama aliye na maambukizi ya Hepatitis B.
Inasemekana kuwa endapo hakuna juhudi za matibabu za mapema za kuzuia maambukizi kuna uwezekano wa hadi asilimia 90 kwa mama kumuambukiza mtoto.
Kutokana na tatizo hilo, Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto kutoka kituo cha Afya cha Mji kilichopo Manispaa ya Lindi (LINDI MC), Farida Ibrahimu anawashauri akina mama kuwahi kliniki pindi wanapojihisi kuwa ni wajawazito ili waweze kupata chanjo ikiwamo ya homa ya ini pamoja na ushauri wa afya ya uzazi kuepukana na changamoto za maradhi kwa watoto watakaozaliwa.
Mratibu huyo amesema mama kuwahi kliniki pindi tu anapojihisi kuwa ni mjamzito, kulingana na vipimo vya awali atakavyofanyiwa ataweza kujua kama ana maambukizi ya aina yoyote ambayo yanaweza kumuathili mtoto alie tumboni, hivyo kuweza kumlinda mtoto huyo kitaalamu mpaka atakapozaliwa.
“Katika maeneo hatari zaidi duniani virusi vya hepatitis B kwa kawaida usambazwa kupitia kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua au kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine hususani nyakati za utotoni “iwapo hamna juhudi za kitiba za kuzuia maambukizi kuna uwezekano hadi asilimia 90 kwa mama alie na maambukizi kumuambukiza mtoto wakati wa kujifungua.
Anasema kama ilivyo kwa virusi vya UKIMWI, virusi vya homa ya ini pia uambukizwa kwa njia ya kujamiiana, mate,jasho na mwingiliano wa damu ya mtu mwenye virusi, hivyo endapo mama mjamzito hatapata chanjo na ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya ni rahisi kwa mtoto atakaejifungua kupata maambukizi hayo.
Kwa mujibu wa taarifa ya tovuti ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine, inaonyesha homa ya ini ni janga linaloua kimya kimya ambapo kulingana na takwimu za vifo duniani inakadiliwa ugonjwa huo unaua watu 600,000 kila mwaka.
Kwa wastani watu zaidi ya bilioni mbili, sawa na asilimia 33 ya watu wote ulimwenguni, wameambukizwa virusi vya HBV na wengi wao hupona baada ya miezi michache, huku watu milioni 350 wakiendelea kuwa na virusi hivyo mwilini ambapo wengi huishi bila dalili na kuendelea kuambukiza watu wengine.
Katika maeneo ya Bara la Afrika ikiwamo Tanzania, maambukizi ya virusi vya homa ya ini ndio sababu kuu ya kuleta shida kwenye ini.
Virusi vya homa ya ini vipo vya aina tano yaani A,B,C,D, na E ingawa aina mbili za virusi hivyo B na C ndio sababu kuu ya ugonjwa wa homa ya ini na kusambaa kupitia damu na maji maji ya mwili.
Taarifa hiyo inasema kuwahi kituo cha cha afya mapema kwa mama mjamzito hasa mwenye maambukizi ya ugonjwa huo wa ini pindi tu anaposikia hali ya uchungu ni muhuhimu ili wataalamu kuweza kufanya maandalizi ya awali kwa ajili ya kumkinga motto.
Naye muuguzi mkunga katika kituo hiko cha Afya cha Mji, Grecy Mrope,
anaeleza kuwa mama mjamzito anaweza kumkinga mtoto wake asipate ugonjwa huo pale wahudumu au wataalamu wanapompatia huduma kipindi cha kujifungua kwa njia ya kawaida au upasuaji.
Anasema mtoto akishazaliwa anatakiwa kupewa dozi ya Heptitis B, ndani ya masaa 12 ili kumkinga na homa ya ini.
huku akieleza kuwa dozi hiyo inatakiwa apewe mara tatu, ambapo dozi ya kwanza atapatiwa ndani ya masaa 12 tangu azaliwe, ya pili baada ya miezi sita na dozi ya mwisho ni baada ya mwaka mmoja.
Pamoja na ugonjwa huu kuwa hatari na virusi vyake kusambaa na kuambukiza mtu mara 100 zaidi ya virusi vya UKIMWI kama ilivyoelezwa katika tovuti ya Hospitali ya Mkoa wa Lindi Sokoine bado elimu juu ya homa hiyo haijafikishwa vya kutosha.
Shuwea Juma mkazi wa Manispaa ya Lindi anasema pamoja na ugonjwa huo wa ini kuwa ni hatari lakini bado elimu ya kutosha kuhusiana haijafika kwa wananchi.
“Mimi nadhani elimu izidi kutolewa zaidi kwa wananchi juu ya ugonjwa huu kupitia kwenye vyombo vya habari hata mbao za matangazo na hata mashuleni kama ilivyo kwa magonjwa mengine kama vile UKIMWI ili wananchi tuchukue tahadhari zaidi za ugonjwa huo,” anaeleza Shuwea.