Na PENDO FUNDISHA, MBEYA
MAELFU ya watu kutoka ndani na nje ya nchi, jana walishuhudia tukio la kupatwa kwa jua katika eneo la Rujewa, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya.
Jua lilianza kupatwa jana saa 4:15 asubuhi hadi saa saba mchana baada ya kuonekana limefunikwa na mwezi.
Baada ya hatua hiyo, hali ya hewa ilibadilika ghafla. Ilitokea baridi kali, huku eneo lote likionekana kutawaliwa na giza.
Akizungumzia hali hiyo, mtaalamu wa anga na nyota kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk. Noolali Jihali, alisema tukio hilo linatokana na hali ya kisayansi ambayo hutokea kila baada ya miaka 15.
“Mwaka 1977 jua lilipatwa na leo hii (jana) limepatwa pia na litapatwa tena mwaka 2032.
“Tukio la aina hii hutokea zaidi katika maeneo yaliyo na hali ya hewa yenye joto na anga angavu kama lilivyo eneo la Rujewa na Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe ambako ndiko kuna asilimia kubwa za kuona jua jinsi linavyopatwa kwa kutumia kifaa kinachochuja mionzi ya jua.
“Kifaa hicho kina uwezo mkubwa wa kuchuja mionzi ya jua kwa asilimia 99.99 na hiyo ndiyo sababu ya wananchi kutakiwa kutumia kifaa hicho kwa kutazama kwani kina uwezo mkubwa wa kupunguza madhara kwenye macho,” alisema Dk. Jihali.
Akizungumzia tukio hilo, Katibu wa Mila wilayani Mbarali, Mwanasimtwa Mwagongo, alisema miaka iliyopita tukio hilo lilipokuwa likitokea, wazee walikuwa wakichinja ng’ombe kama sehemu ya tambiko kwani walikuwa wakiamini huo ni mkosi kwa nchi.
“Lakini hivi sasa wengi wameelimika na kulitambua tukio hilo kwamba ni la kisayansi, ingawa bado tunaamini ni neema kwa eneo lilikotokea tukio hilo.
“Hata hivyo, napenda kuwaonya waganga wa jadi wasitumie kupatwa kwa jua kwa masilahi yao binafsi kwani wanaweza kuwaaminisha kwamba wao ndio waliosababisha jua lisiendelee kupatwa.
“Nasema hivyo kwa sababu tayari tumeshaanza kusikia taarifa kwamba kuna baadhi ya waganga wa jadi wameanza kuwaambia wananchi eti tukio hilo linapotokea na kusababisha giza, basi hali ya mwanga haitatokea tena mpaka wao wafanye utaalamu wao jambo ambalo si kweli.
“Wananchi waelewe kwamba tukio la kupatwa kwa jua au kupatwa kwa mwezi ni la kitaalamu na haliingiliani kabisa na imani za kienyeji,” alisema Mwagongo.
Pamoja na hayo, alisema kitendo cha kuonekana kwa jua likipatwa wilayani Mbarali, ni mwendelezo wa uwepo wa utalii wilayani hapa kwa kuwa kuna vivutio vingi vya kitalii, ikiwamo nyumba iliyohifadhi mwili wa Chifu Melele iliyokuwa na ngome iliyotumiwa na Wangoni wakati wa vita vya kumwondoa mkoloni.
Wakati huo huo, jana mji wa Rujewa ulikuwa na sura ya pekee kutokana na wingi wa wageni waliofika kushuhudia tukio hilo.
Nyumba za kulala wageni, zote zilijaa na kusababisha baadhi ya wageni kulala kwenye mahema. Biashara mbalimbali nazo zilifanyika huku bei za vyakula zikipanda mara dufu.
Bei ya sahani ya wali ambayo huuzwa kwa Sh 2,500 ilipanda hadi Sh 5,000 na bei ya kikombe cha chai ambacho huuzwa kwa Sh 500 ilipanda hadi Sh 600.
Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari mkoani Mbeya nao hawakubaki nyuma kwani walikuwa eneo la tukio wakiwa na walimu wao wakisoma tukio hilo kwa vitendo.
Akizungumzia tukio hilo, mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Uwata, Maria Kabuje, alionyesha kufurahia na kusema ni mara yake ya kwanza kushuhudia jua likipatwa.