25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JINSI HOJA NANE ZILIVYOTIKISA BUNGE


Na FREDY AZZAH-DODOMA   |

ZIKIWA zimepita siku nne tu kati ya zaidi ya 80 za mkutano wa 11 wa Bunge la 11 kujadili bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19, takribani mambo nane yametikisa ikiwa ni pamoja na wapinzani kususa kusoma bajeti mbadala na wabunge wakiwararua mawaziri bila kujali vyama vyao.

Mkutano huu tunaweza kusema umeanza kivingine kutokana na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), kugoma kusoma bajeti mbadala kutokana na madai ya watumishi wake waliokuwa wakifanya kazi ya utafiti, kuchambua sheria na kuandaa hotuba zao kufukuzwa na Bunge.

Tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesoma hotuba makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake huku Kiongozi wa KUB, Freeman Mbowe, akishindwa kusoma bajeti mbadala kwenye ofisi hiyo.

Awali Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema hotuba hiyo ya upinzani haijasomwa kwa sababu wameshindwa kuiwasilisha siku moja kabla kama waraka wa Spika unavyoelekeza.

Hata hivyo, Mbowe alitoa ufafanuzi na kusema kushindwa kwao kusoma hotuba ni kwa sababu watumishi hao wa upinzani ambao wanatakiwa kulipwa na Bunge kwa mujibu wa kanuni, walifukuzwa kwenye ofisi hizo hivyo hakuna mtu wa kufanya utafiti na kuandaa hotuba hizo.

Kutokana na hali hiyo, alisema KUB haitasoma bajeti mbadala hadi pale vijana hao watakaporudishwa na pia hata wakirudishwa, hawatakubali kuziwasilisha kwa Spika waambiwe nini cha kusoma na cha kutoa.

KUB wamekuwa wakishindwa kusoma bajeti mbadala kwa sababu ya kususa vikao vya Bunge, lakini hii ni mara ya kwanza kwa wabunge wa kambi hiyo kuwa bungeni na kutosoma bajeti mbadala.

Hoja zilizotikisa

Katika siku tatu za kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu, baadhi ya hoja kubwa zilizoibuliwa na wabunge ni pamoja na wavuvi kuonewa katika operesheni ya kutokomeza uvuvi haramu, watumishi wa umma wenye elimu ya darasa la saba kufukuzwa na usalama kwa raia.

Pia suala la sukari ya Zanzibar kukatazwa kuuzwa nchini, Serikali kutenga fedha za kununua chakula na Msajili wa vyama vya siasa kuzorotesha demokrasia.

Hoja iliyochangiwa na wabunge wengi zaidi ni ile ya Serikali kufukuza watumishi wenye elimu ya darasa la saba, ambayo ilimfanya Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku (Musukuma), kutaka warejeshwe kazini vinginevyo wabunge wenye elimu hiyo nao wafukuzwe bungeni.

 

Alisema wabunge hao wakishaondolewa bungeni, waingie tena kwa tiketi ya viti maalumu kama ilivyo kwa wanawake na walemavu, ili wawatetee watu wenye elimu ya darasa la saba aliodai ni zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania.

Wabunge wengi waliochangia hoja hiyo walisema, wanashangaa kuona hata madereva wakifukuzwa kwa kuambiwa wana elimu ya darasa la saba huku fani hiyo ikihitaji zaidi ujuzi kuliko elimu ya darasani.

Walisema pia madereva wengi waliofukuzwa walibakisha muda mfupi wastaafu hivyo kushauri warudishwe kazini hadi wastaafu na mfumo mpya utumike kwa waajiriwa wapya.

Kwa upande wa wavuvi kuonewa, hoja hiyo ilichangiwa zaidi na wabunge wa Kanda ya Ziwa, ambao walisema mbali na wavuvi, wananchi wao pia wanateseka kwa kukosa kitoweo na biashara.

Walisema zoezi hilo linaendeshwa zaidi kwa kukomoa badala ya kufuata taratibu na sheria.

Mbunge wa Geita (CCM), Costantine Kanyasu, alisema nyavu ambazo zimeruhusiwa na Serikali zinaweza kukamata samaki wadogo kuliko wale walioruhusiwa lakini bado wavuvi wakikutwa nao wanaonewa.

Suala la sukari la Zanzibar kutouzwa Bara, lilizua mjadala ambapo wabunge kutoka kisiwani humo walisema kuendelea marufuku hiyo ni kudhoofisha Muungano.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ali Kessy, alisema wafanyabiashara wa Zanzibar wamekuwa wakiagiza nje na kuilipia kodi ndogo na baadaye kutaka kuingiza Bara jambo alilosema kulifanya eneo hilo kuwa jalala.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashantu Kijaji, alijibu hoja hiyo kwa kusema: “Kiwanda cha Zanzibar kina uwezo wa kuzalisha tani 8,000 za sukari kwa mwaka wakati mahitaji ya Zanzibar na Bara ni tani 17,000 hadi 20,000, kwa hiyo msemaji ajielekeze kwenye hoja asipotoshe wananchi.”

Ukiacha hoja hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani, walisema Msajili wa vyama vya siasa anachangia kuua vyama badala ya kuvilea kama ilivyo jukumu lake.

Hoja hiyo ilitanguliwa na ile iliyozua mjadala iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa, ambaye aliiagiza ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kutosita kufuta chama chochote cha siasa kinachokiuka sheria, kanuni na taratibu za uendesheji wa vyama vya siasa nchini.

Mbunge wa Chambani (CUF), Yusufu Salum Hussein, yeye alimshutumu Msajili akisema: “Ndiye anaua demokrasia hasa vyama vya upinzani, leo ndiyo anaiandikia barua Chadema ili wajieleze kwanini wasichukuliwe hatua kwa sababu ya kuandamana, kwani nchi hii kuandamana ni haramu.”

Naye Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hillary (CCM), aliibua suala la hifadhi ya chakula huku akishangazwa na Serikali kutenga Sh bilioni 15 kati ya Sh bilioni 80 walizoombwa na Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA) na kusema mwaka huu Serikali ikifunga mipaka ya nchi ili chakula kisiuzwe nje, watashikana mashati bungeni.

Suala la usalama wa raia pia liliibuka ambapo baadhi ya wabunge waliitaka Serikali iimarishe ulinzi kwa wananchi na kutokomeza aina zote za uonevu.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), aliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuunda chombo maalumu kitakachochunguza mauaji ya muuza machungwa, Allen Mapunda (20), aliyefariki mkoani Mbeya hivi karibuni kwa kile kinachodaiwa kupigwa na polisi.

Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaa Nachuma, naye alitaka iundwe timu ya kuchunguza kifo cha kijana aliyeuawa Mtwara na polisi wakati akijitafutia kitoweo baharini.

Mbali na hoja hizo, wiki ya kwanza ya mkutano huu, imeshuhudia idadi ndogo ya mahudhurio ya wabunge kwa pande zote.

Siku mbili za kwanza upinzani na hasa Chadema, mahudhurio yao yalikuwa chini zaidi na baadaye Mbowe akaja kusema walikuwa wanasubiri kwanza kuweka msimamo kama kambi namna watakavyoshiriki Bunge hilo.

Akitoa maombi ya bajeti yake Aprili nne, Waziri Mkuu Majaliwa, aliomba Bunge kuidhinisha Sh bilioni 124.954 kati yake Sh bilioni 66.162 ni matumizi ya kawaida na Sh bilioni 58.791 ni matumizi ya maendeleo.

Pia alitaka Bunge kuidhinisha Sh bilioni 125.521 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge kati yake Sh bilioni 117.205 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh bilioni 8.315 matumizi ya maendeleo.

Katika mwaka wa fedha utakaoisha Juni 31, Ofisi ya Waziri Mkuu iliomba kuidhinishiwa Sh bilioni 171.66 huku Ofisi ya Bunge ikiidhinishiwa Sh bilioni 121.65.

Ajira

Akizungumzia ajira, Majaliwa alisema hadi Februari 2018, ajira 482,601 zilikuwa zimezalishwa kwenye sekta rasmi kati yake 345,547 sawa na asilimia 72 zikiwa zimezalishwa na Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles