30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

JINSI DAWA ZA KULEVYA ZINAVYOITIKISA DUNIA

Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM  

KAMPENI ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya iliyoanzishwa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kabla ya kupokewa na kuanza kutekelezwa chini ya mfumo rasmi wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa hizo, imekuja wakati ambao si tu Tanzania bali dunia ikiwa hatarini kutokana na kuongezeka kwa watumiaji wa kilevi hicho.

Ripoti iliyotolewa mwaka jana ya Kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachojihusisha na mapambano ya dawa za kulevya (UNODC), inaonyesha kuwa katika watu wazima 20, mmoja anatumia dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya watu milioni 29 hawako sawa sawa kiafya kwa sababu ya matumizi ya dawa za kulevya, huku bangi ikielezwa kubaki kama kilevi kinachotumika sana, ikikadiriwa watu milioni 183 wanatumia hadi kufikia mwaka 2014.

Pamoja na hayo, kwa muda mrefu ripoti zimekuwa zikizitaja nchi za Kenya na Tanzania kwa upande wa Afrika Mashariki kama kiunganishi kikuu cha usafirishaji wa dawa za kulevya kutoka Afghanistan kwenda katika bara la Ulaya.

Inaelezwa dawa nyingi aina ya heroin kutoka Afghanistan husafirishwa kwenda Ulaya kwa njia kuu mbili; ya kwanza ikiwa ya kupitia bara la Asia la kati na nyingine ni ya Mashariki kupitia nchini Iran.

Gazeti maarufu la nchini Uingereza, The Economist, mwaka jana liliwahi kuripoti kuwa njia ambayo imekuwa ikitumika kupitisha dawa hizo kwa upande wa Afrika Mashariki imekuwa ikitumika tangu mwaka 1980.

Ripoti ya UNODC ya miaka miwili iliyopita, ilieleza kuwa tangu kuanza kwa ukamataji wa dawa za kulevya mwaka juzi ambapo kiasi cha kilogramu 3,500 zilizokuwa zikisafirishwa zilikamatwa, biashara hiyo bado inaendelea kukua.

Mmoja wa wasemaji  kutoka UNODC, Alan Cole, aliwahi kukaririwa na The Economist akisema kuhama kwa njia kuu za usafirishaji kwenda Afrika Mashariki na nyingine kulitokana na kuwapo kwa marekebisho ya sheria  huko Ulaya ya Kati na machafuko yaliyoko Syria.

The Economist liliandika kuwa upekuzi mkali unaofanywa katika mipaka pembezoni mwa njia ya Balkan na wasafirishaji kuhofia kukamatwa kwa uchochezi wa vita katika Mashariki ya Kati vimesababisha  njia hiyo kuwa si kivutio tena.

Inaelezwa badala yake, wafanyabiashara hao wa dawa za kulevya wamehamia njia za baharini.

Katika usafirishaji wa heroin kwa njia ya bahari, dawa hizo hupakuliwa kutoka katika majahazi na meli  hadi kwenye fukwe za nchi za Kenya na Tanzania na kuwekwa ndani ya boti ndogo zenye mwendo mkali ambazo huwa ufukweni mwa bahari.

Jarida hilo la nchini Uingereza katika ripoti yake hiyo liliandika kuwa nchini Kenya, na Tanzania makundi ya wauza dawa hizo wanaunda ukaribu na baadhi ya wanasiasa mashuhuri na maofisa wa usalama ambao wamekuwa wakilinda biashara hiyo.

The Economist lilidai kuwa hata huvyo wanasiasa hao wanajihatarisha iwapo hawatakuwa madarakani au inapotokea wanamtandao huo wanapokamatwa.

Moja ya tafiti zilifanywa mwaka 2011 na shirika moja la kimataifa la amani lililopo jijini New York nchini Marekani, uliripoti kuwa  wafanyabiashara  wakuu kutoka nchini Kenya wanahusika na biashara hiyo.

Mwaka huohuo, Marekani ilichagua  watu saba akiwamo Mbunge kutoka Kenya,  John Harun Mwau, kama mmoja wa wahusika wakuu wa dawa hizo za kulevya ambaye ilizuia vyanzo vyake vyote vya mapato nchini humo ikiwamo pia kumwondoa kwenye mfumo wa fedha. Mwau alikana mashtaka hayo na kudai kuwa nchi ya Marekani imekuwa ikijaribu kuzuia uendeshaji wa biashara zake za maduka makubwa (Supermarkets) ambazo alidai zilimwingizia faida kubwa.

Wakati nchini Tanzania kampeni hii ikifufuliwa upya na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda na kuibua vita ya maneno, hasa kati yake na wanasiasa, nchini Kenya nako hali hiyo imejitokeza baada na wao kuendesha kampeni hiyo.

Miaka miwili iliyopita,  Rais Uhuru Kenyatta alitoa amri ya kukamatwa kwa meli iliyokuwa imebeba heroin na mzigo wote kuharibiwa kinyume na amri iliyotolewa na Jaji Mkuu wa Mombasa na hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ambayo ilikuwa ikisikiliza kesi ya dawa za kulevya iliyohusisha watu tisa waliokamatwa katika meli hiyo.

Meli hiyo ya MV Al Noor, ambayo ilikuwa imetokea ufukwe wa Makran, Kusini Mashariki mwa Pakistan, ilikamatwa na wanajeshi wa majini wa Magharibi (Western naval forces) ambao walikuwa wakilinda usalama katika bahari ya Hindi kwa nia ya kutokomeza maharamia kutoka Somalia na  biashara ya usafirishaji wa binadamu.

Si hayo tu, nchi za Mashariki pia zimekuwa zikitiliwa shaka kuhusu biashara ya usafirishaji dawa za kulevya aina ya cocaine ambayo imeendelea kushamiri katika miaka ya kati ya 2000.

Mbali na Tanzania na Kenya ambako inaelezwa mara tu mamlaka zilipoanza kuwa mstari wa mbele kukamata na kutokomeza biashara hiyo, katika bahari ya Atlantiki, maharamia walihamia kwenye njia za kuelekea kusini mwa Afrika ya Magharibi, ambako ndiko kwenye mataifa yaliyo dhaifu na rahisi kuingilika, yanayoendekeza rushwa na kujali zaidi kujipatia pesa kwa njia ya biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya.

Nchi hizo ni pamoja na  Ghana, Mali na  Senegal ambazo ripoti bado zinataja kuwa zimeendelea kuwa njia kuu na vituo vya usafirishaji wa dawa hizo za aina ya cocaine  kwa njia ya baharini kutokea Amerika ya Kusini tayari kusafirishwa kwenda bara la Ulaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles