NA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM
HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imeingia kwenye mgogoro na Manispaa ya Ilala baada ya kila mmoja kudai kuwa ana haki ya kukusanya mapato yatokanayo na biashara ya taksi.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe, alisema kuanzia sasa mapato hayo yatakusanywa na ofisi yake na kudai kuwa Manispaa ya Ilala haina haki hiyo kwa mujibu wa sheria.
Mgogoro huo umedumu mpaka sasa, huku Umoja wa Madereva Taksi Manispaa ya Ilala (UMATAWI), ukisema uko njia panda kutokana na kushindwa kujua wapi wanatakiwa kwenda kulipa kodi hiyo.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa UMATAWI, Abbas Iddi, alisema waliambiwa mwaka huu wakalipie Jiji, lakini wameshangaa kuona Manispaa ya Ilala ikipita na kutoa matangazo ya kuwataka wakalipie kwao.
“Wanapita wanatutangazia tukalipe Manispaa na wametoa muda hadi mwisho wa mwezi huu ndiyo mwisho. Tumekwenda Jiji wanatuambia tusubiri bado wanalishughulikia suala hili, sasa tunakosa mwelekeo tukalipe wapi,” alisema Iddi.
Juni 26 mwaka huu, Manispaa ya Ilala ilitoa tangazo la kuwataka madereva wote kwenda kulipia na kwamba kuanzia Agosti Mosi mwaka huu wataendesha msako wa kuwakamata ambao hawajalipia.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, mapato yanayotakiwa kulipwa ni Sh 61,000, ambazo zinajumuisha usajili wa gari Sh 20,000, ada ya maegesho Sh 36,000 na ada ya kituo Sh 5,000.
Hata hivyo, siku chache baada ya tangazo hilo, Mkurugenzi wa Jiji naye alitoa tangazo la kutaka vituo vyote vya taksi visubiri utaratibu utakaoandaliwa.
“Matangazo yote yaliyotolewa na Manispaa ya Ilala kuhusu maegesho ya taksi ni batili. Vituo vyote vya taksi visubiri utaratibu utakaoandaliwa na Halmashauri ya Jiji. Maegesho yote ya magari yako chini ya Halmashauri ya Jiji kwa mujibu wa sheria ndogo ya maegesho GN namba 60 ya mwaka 1998,” ilisema sehemu ya tangazo hilo la Jiji.
Kwa mujibu wa UMATAWI, hadi sasa kuna vituo vya taksi 178 na kila kituo kina magari kati ya 6 hadi 40.
Mmoja wa madereva wa taksi, Jacob Anyandwile, alisema wao wanapendekeza kwenda kulipa Jiji kwa sababu limeonyesha ushirikiano mkubwa kwao.