24.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 30, 2023

Contact us: [email protected]

Jiji lasema bajeti haitoshi mikopo ya vikundi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imesema bado haijaweza kukidhi mahitaji ya vikundi vyote vinavyohitaji mikopo vikiwemo vya watu wenye ulemavu kwa sababu bajeti inayotengwa haitoshelezi.

Mwandishi wa habari hii akizungumza na Maulid Kibangala.

Katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 halmashauri hiyo imetoa mikopo kwa vikundi 560 na kati ya hivyo vikundi vya watu wenye ulemavu ni 69.

Akizungumza na Mtanzania Digital, Ofisa Uhusiano wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Tabu Shaibu, amesema vikundi vinavyohitaji mikopo ni vingi ndiyo maana huwa wanatoa kwa awamu.

“Hizi fedha huwa tunatenga asilimia 10 tu ya mapato yetu ya ndani kama mwongozo unavyosema lakini vikundi vinavyoomba ni vingi, kikubwa tunachosisitiza ni urejeshaji ili wengine waweze kukopa,” amesema Tabu.

Amesema katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 6.3 kwa vikindi 560.

Maulid Kibangala.

Idadi ya vikundi na kiasi cha fedha kwenye mabano ni vikundi vya wanawake ni 290 (Sh bilioni 2.6), vijana vikundi 201 (Sh bilioni 2.6) na watu wenye ulemavu vikundi 69 (Sh bilioni 1).

Maulid Kibangala (29) ambaye ana ualbino anajishughulisha kuendesha bajaji katika eneo la Kariakoo – Soko la Samaki Feri amesema katika kikundi chao wameomba mkopo lakini mpaka sasa bado hawajapata.

Amesema kama angefanikiwa kupata mkopo wa bajaji ndani ya mwaka mmoja angeweza kununua chombo chake mwenyewe na kuepuka usumbufu wa waajiri.

“Kama kwa siku napata Sh 40,000 bosi nampa Sh 15,000, mafuta Sh 10,000 nabakiwa na Sh 15,000 nina uwezo wa kununua bajaji yangu. Hawa mabosi wakati mwingine unaweza kwenda kuchukua chombo anakuambia leo ‘usiamshe’ au chombo kinaweza kuwa kibovu lakini hatengenezi, lakini ukiwa na bajaji yako ikiharibika lazima utatengeneza na utapiga hatua,” amesema Kibangala.

Ameshauri pia kwa mikopo ya vyombo vya moto kama vile bajaji ni vema kila mwanakikundi akakopeshwa ya kwake kwani itasaidia kutunza vizuri tofauti na sasa ambapo kikundi cha watu saba kinaweza kukopeshwa bajaji tatu.

Ofisa Uhusiano wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Tabu Shaibu.

Kibangala amesema kazi ya kuendesha bajaji imebadili maisha yake tofauti na awali alipokuwa akifanya biashara ndogondogo za kuuza pipi, karanga, sigara na genge.

“Kazi hii inanisaidia tofauti na zamani kwa sababu biashara ndogondogo zinahitaji mtaji lakini kwenye bajaji ni Sh 10,000 tu ya mafuta, kwahiyo mambo madogo madogo naweza kuyatatua,” amesema.

Kibangala ambaye ana mke na mtoto mmoja anayesoma darasa la tano, amesema licha ya kukidhi mahitaji ya familia kazi hiyo pia imemuwezesha kununua kiwanja na matofali.

Hata hivyo amesema changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni kudharauliwa na watumiaji wengine wa barabara na baadhi ya abiria wanaowapakia kwa kile alichodai kuwa si wastarabu.

“Wenye magari wanatudharau wenye bajaji hajui inaendeshwa na mtu aliyeenda Veta, anaweza kukuchomekea unajikuta unaenda pembeni. Baadhi ya abiria nao akishatoa Sh 1,000 anajiona ana haki zote kuliko mwendesha bajaji…unamuuliza unashuka wapi anakujibu ovyo wanachukulia kama sisi ni wahuni,” amesema Kibangala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,203FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles