22.7 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Jiji la Arusha linavyolia na anguko la utalii

t1

NA JUSTIN DAMIAN,

WAKATI ripoti mbalimbali zikiwamo zile za kiuchumi zinazotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zikionyesha kukua kwa uchumi wa nchi, hali halisi mitaani inatoa picha ya tofauti kabisa.

Wiki tatu zilizopita, nilikuwa mkoani Arusha, mkoa ambao ndio unaongoza kwa shughuli za utalii kutokana na kuwa na vivutio vingi. Nilikuwa mkoani hapo kwa wiki mbili. Nakumbuka mara ya mwisho kufika Arusha  ni takribani miaka minne iliyopita na hali niliyoikuta ilikuwa tofauti na niliyoiacha.

Mkoa wa Arusha wa miaka minne iliyopita ulikuwa ulikuwa umechangamka na uliokuwa na pilika nyingi za shughuli za kiuchumi ambazo kwa kiasi kikubwa zilichagizwa na utalii.

Kwa ambao wamefika mkoani Arusha watakubaliana na mimi kuwa, mandhari ya mji huo wa kitalii inapambwa na majengo marefu na ya kifahari ambayo mengi ni hoteli.

Nilishangazwa kuona na kuelezwa na wenyeji kuwa, baadhi ya hoteli maarufu kama Mount Meru na Snow Crest zimeshindwa kujiendesha na kuamua kufunga biashara huku baadhi zikielekea kugeuka magofu kutokana na kuachwa bila uangalizi wowote.

Nilipojaribu kuingia kwenye sehemu za burudani kama mabaa na nyinginezo, sikuziona shamra shamra za Arusha niliyoiacha miaka minne iliyopita.

Wenyeji wangu waliniambia kuwa mzunguko wa fedha katika jiji hilo la kitalii umekuwa mdogo sana kutokana na kuzorota kwa shughuli za utalii ambazo kwa kiasi kikubwa ndiyo zinalifanya kuwa na mzunguko wa fedha.

Waliniambia kuwa, sekta ya utalii ilikuwa imeajiri vijana wengi lakini baada ya kuanguka vijana hao hawana kazi na baadhi yao wameanza kujihusisha kwenye vitendo vya uhalifu ili kujikimu kimaisha kwa kuwa hawana kazi.

Itakumbukwa kuwa, Chama cha Mawakala wa Utalii Kanda ya Kaskazini (Kiato), kiliwahi kuionya Serikali kuwa kitendo cha kuweka Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), katika sekta ya utalii, kingeweza kupunguza idadi ya watalii nchini na ndicho kilichotokea Arusha.

Chama hicho kilisema kutokana na gharama kubwa wanazolipa watalii, Serikali haipaswi kuongeza kodi nyingine kwa kufanya hivyo itaua sekta ya utalii ambayo inaliingizia taifa fedha nyingi za kigeni. Utalii kwa sasa unachangia asilimia 16 ya pato la taifa.

Mmoja wa kijana ambaye alikuwa akiwaogoza watalii, alinieleza kuwa kampuni za kitalii yakiwamo mahoteli yameshindwa kujiendesha kutokana na kukosa wateja jambo ambalo linawalazimu kufunga biashara.

Katika mazingira kama haya ukielezwa uchumi unakua tena kwa kasi inakuwa vigumu kukuingia akilini. Mimi si mchumi lakini nitajaribu kuchambua suala hili kwa kuangalia maisha ya kawaida ya Mtanzania.

Uchumi ambao Watanzania wengi wangeutamani ni ule unaowanufaisha wananchi walio wengi, uchumi unaowawezesha kupata ajira, kufanya biashara pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi ambazo zitawezesha kuwa na kipato cha kuendesha maisha yao.

Wakati mwingine napata hisia kuwa, pengine wachumi wetu hawamshauri vizuri Rais ambaye ameonyesha nia ya dhati ya kuhahakikisha kuwa uchumi unaokuwa unamnufaisha mwananchi wa chini kabisa.

Sioni kama ni jambo jema sana kuongeza kodi kubwa kwenye utalii kutokana na ushindani uliopo. Wakati Tanzania ikiongeza gharama nchi jirani ambao ni washindani wanachukulia kama fursa kwao. Athari ya jambo hili linaonekana wazi katika mji wa Arusha.

Binafsi siamini kama Rais anapenda kuona nchi ambayo inataka ijitegemee ikishindwa kufanya hivyo. Hao waliompelekea pendekezo la kuongeza kodi kwenye utalii ikiwa ni moja ya eneo la kuongeza wigo wa vyanzo vya mapato inawezekana hawakuifanya kazi hiyo kwa kuliangalia jambo hilo kwa mapana yake.

Sekta ya utalii ni moja kati ya sekta ambazo zina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi kutokana na mapato pamoja na kutengeneza ajira.

Katika muktadha huu, ilikuwa ni muhimu kubuni mbinu ambazo zingewavutia watalii wengi na si kuongeza gharama ambazo zitawakimbiza.

Maamuzi yanapofanyika wakati mwingine ni muhimu kuangalia nchi nyingine ambazo zimefanikiwa badala ya kujifungia ndani na kuja na maamuzi ambayo hayana tija.

Uamuzi wa kuongeza kodi kwenye utalii tayari umesababisha baadhi ya Watanzania kupoteza ajira zao. Gazeti moja linaloandika kwa lugha ya Kiingereza na kuuzwa katika nchi za Afrika Mashariki limewahi kuandika kuwa, kuna uwezekano mkubwa kwa sekta ya utalii kuanguka vibaya kutokana na uamuzi wa kuongeza kodi.

Hakuna binadamu aliyemkamilifu na ni vyema pale tunapokosea tukakubali kuwa tumekosea na kujirekebisha.

Tusipokubaliana na kujirekebisha uchumi utaendelea kuwanufaisha watu wachache jambo ambalo si lengo la nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,580FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles