28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Jiji la Arusha kuzindua mradi wa matofali

Janeth Mushi, Arusha

Katika kupunguza gharama za ujenzi katika utekelezaji wa  miradi yake ya ndani, Halmashauri ya Jiji la Arusha imeanzisha mradi maalum wa kutengeneza matofali.

Mradi huo uliopo mbioni kukamilika na utakaozinduliwa hivi karibuni,umejengwa katika Kata ya Lemara,ambapo miradi yote ya ndani katika halmashauri hiyo itanunua matofali kutoka katika eneo hilo.

Kamati ya fedha ya jiji hilo ikiongozwa na Meya wake  Maxmillian Iranghe na Mkurugenzi wa Jiji hilo Dk. John Pima leo wamefika katika eneo hilo na kukagua mradi huo.

Mkuu wa idara ya uchumi katika Jiji hilo, Mathias Shindika,anasema mradi huo utakaopunguza gharama za ujenzi wa miradi ya serikali unatarajiwa kuzalisha matofali 6,000 kwa siku.

“Mradi utakuwa chanzo cha mapato katika jiji letu na lengo la kuwa na mradi ina maana miradi yote iliyopo chini ya jiji itapata matofali katika eneo hilo,”anasema.

“Mwanzoni tulikuwa tunanunua matofali kwa watu binafsi kwa gharama kubwa,lakini kwa kiwanda hiki kitatusaidia kupunguza gharama za ujenzi katika miradi yetu ya halmashauri.

“Lakini pia bidhaa zinazozalishwa hapa zina ubora kwa sababu tunasimamia sisi wenyewe kama halmashaui na wateja wengine ni taasisi na watu binafsi tunawategemea,”ameongeza.

Mkuu huyo anasema wanatarajia kwa makadirio ya chini kukusanya Sh milioni 86 kwa mwezi kupitia mradi huo.
 Kwa upande wake Dk. Pima, amesema wanatarajia kuzindua mradi huo hivi karibuni baada ya kukamilika kwake na kuwa watahakikisha wanasimamia mradi huo ili uwe na matokeo chanya.

Amesema kuwa mradi huo utasaidia kuongeza mapato katika halmashauri hiyo na kufanikisha ujenzi wa miradi yake mbalimbali.

 Naye Meya Iranghe,amepongeza kamati hiyo ya fedha kwa kupitisha mradi huo ambao wanautarajia uwe wenye tija na kuwa watauendesha kwa faida.

“Hapa inabidi ifanyike kama biashara nyingine yoyote shule ikitengewa fedha ije kununua matofali hapa kwa sababu vinginevyo tukisema tunachukua kwa sababu ni mradi wetu tutashindwa hata kuuendesha.

“Nasisitiza hili kwani miradi mingi ya serikali wakati mwingine inashindwa kusonga kwa sababu ya uendeshaji hivyo wataalamu wa halmashauri hasa wahandisi  tunzeni huu mradi,”.

Diwani wa Kata ya Lemara,Naboti Silas,ameshukuru uwepo wa mradi huo katika eneo hilo na kuwa wanatarajia kupata manufaa mengi ikiwemo ajira zitokanazo za mradi huo.
 
“Binafsi nishukuru kwa mradi kuwepo kwenye kata hii kwani tutapata manufaa mbalimbali ikiwemo ajira  lakini imesogeza huduma kuwa karibu,”amesema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles