JEZI YA AUBAMEYANG YASUMBUA GABON

LIBREVILLE, GABON


Pierre Emerick AubameyangMASHABIKI nchini Gabon wameonekana kuvutiwa na uwezo wa mchezaji wao ambaye ni nahodha wa timu hiyo, Pierre Emerick Aubameyang, hivyo kuwafanya wavae jezi yake mitaani.

Nyota huyo alikuwa wa kwanza kupata bao la kwanza katika dakika ya 53, huku timu yao ikicheza mchezo wa ufunguzi wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Guinea Bissau, ambapo mchezo huo ulimalizika kwa sare ya 1-1.

Mashabiki mbalimbali mitaani wanaonekana wakiwa wamevaa jezi ya nyota huyo, huku wakiamini ndio mchezaji ambaye anaweza kuamua matokeo ya ushindi kwa timu yake akishirikiana na wachezaji wenzake.

Mshambuliaji huyo ambaye anakipiga nchini Ujerumani katika klabu ya Borrusia Dortmund, amekuwa kinara wa kupachika mabao katika Ligi hiyo ya Bundasiliga, hivyo wanaamini hata katika michuano hii anaweza kufanya makubwa kama ilivyokuwa katika ligi yake.

Hata hivyo, kupitia mitandao ya kijamii mashabiki wa nchi hiyo wameonekana kumzungumzia mchezaji wao nyota Aubameyang, kutokana na kiwango alichokionesha kwenye mchezo huo wa kwanza.

Gabon inatarajia kushuka tena dimbani katika mchezo wake wa pili dhidi ya Burkina Faso, mchezo ambao utapigwa kesho kutwa, hivyo wanaamini mchezaji huyo ataanza kuonesha ukali wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here