Mwadishi wetu
Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kimempongeza Rais John Magufuli kwa serikali anayoiongoza kuwa na mikakati kabambe inayoitekeleza ili kuongeza idadi ya watalii kutoka milioni 1.5 ili kufikia watalii milioni 10.
Pongezi hizo zimetolewa leo Alhamisi Desemba 12, na Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, John Chikomo ambapo amesema serikali ya awamu ya tamo imeweza kukomesha ujangili hali iliyopelekea kuwapa wanyama mazingira rafiki ya kuishi.
“Tunachukua fursa hii kwa kweli kupongeza juhudi hizi ambazo JET imezishuhudia katika utekelezaji wa shughuli zake za kuelimisha wananchi wa Tanzania kuhusu utunzaji na uhifadhi wa wanyamapori.
“Kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa JET imetembelea mbuga mbali mbali kama Mikumi, Tarangire, Ruaha, Arusha, mamlaka ya Uhifadhi ya Ngorongoro tumejionea juhudi kubwa ambazo serikali imezifanya kuweka mazingira rafiki kwanza kwa kufikika kwa urahisi kwa maeneo hayo, lakini pia kuboreshwa kwa huduma mbalimbali ambazo zinachagiza watalii kutamani kutembelea maeneo hayo mazuri ya kitalii,” amesema Chikomo.
Ameongeza kuwa juhudi kubwa za kuongeza usafiri wa anga unaofanywa na serikali ya awamu ya tano ni chagizo tosha la kuongeza idadi ya watalii na kuahidi kwamba watatumia weledi wao katika kuhabarisha wananchi ndani na nje ya nchi habari nzuri za maeneo ya kitalii na vivutio ambavyo Tanzania inajuvunia navyo.