29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

JET WAIPONGEZA SERIKALI UTATUZI MIGOGORO YA ARDHI

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), kimeipongeza Serikali kwa juhudi zake za kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, ilieleza kuwa kwa muda mrefu nchi imekuwa ikishuhudia migogoro ya wakulima, wafugaji inayotokana na kugombania ardhi.

Kutokana na hali hiyo, Chikomo alisema kupitia taarifa yake kuwa JET imekuwa ikitetea masilahi ya wakulima masikini na wafugaji nchini dhidi ya wimbi la sasa la wawekezaji wa kigeni na wa ndani kukodishwa ardhi kubwa kwa miaka mingi kwa ajili ya kilimo.

“Katika siku za hivi karibuni, migogoro ya wakulima na wafugaji imekuwa ikiongezeka si tu kwa idadi bali pia kwa madhara yanayotokana na migogoro hiyo. Kadhalika migogoro hii haipo katika sehemu moja ya nchi bali imesambaa karibu nchi yote, hasa katika mashamba ambako pia malisho na maji yanapatikana.

“Vifo, majeruhi, kuchomwa nyumba na kuuawa kwa mifugo ni mambo yanayoashiria ukubwa wa migogoro. Mamlaka kadhaa zimefanya jitihada mbalimbali kutafuta suluhu ya migogoro hiyo lakini mafanikio yamekuwa haba,” alisema Chikomo.

Alisema Serikali za vijiji zimekuwa zikisuluhisha migogoro hiyo hata pale ambapo wameweka mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa kushirikisha makundi yote kama njia mojawapo ya kumaliza tatizo hilo.

Licha ya hali hiyo, alisema migogoro hiyo haiwezi kuachwa ikaendelea kwani pamoja na kugharimu vyakula na mifugo, husababisha uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira hasa pale mifugo inapoingizwa sehemu isiyoruhusiwa na wakulima kuendesha shughuli zao maeneo yaliyozuiliwa.

“Hivyo JET inachukua nafasi hii kupongeza hatua zilizochukuliwa na wakuu wa nchi kwa nia ya kukomesha migogoro hii na kurudisha amani katika maeneo husika ili wananchi waweze kuendelea na kazi zao za kuendesha maisha na kujitafutia maendeleo.

“Kauli ya Rais Dk. John Magufuli kwa wanakijiji cha Fukayosi wilayani Bagamoyo, ikiwemo kuagiza uongozi wa wilaya kuhakikisha kuwa kila mfugaji au mkulima atakayempiga mwingine au kuingilia maeneo yake, ni lazima akamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria,” alisema.

Alisema agizo hilo la Rais Magufuli lilifuatiwa na amri ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyoitoa Wilaya ya Bagamoyo wiki iliyopita, akitaka wale wote wanaopiga wakulima na kuingiza mifigo katika mashamba yao wasakwe, wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Hii ni hatua muhimu iliyochukuliwa na viongozi wakuu wa nchi kwa nia ya kuhakikisha kuwa migogoro baina ya makundi hayo mawili inakomeshwa na amani kurejeshwa.

“Tunawapongeza viongozi wetu kwa hatua hiyo na nyinginezo walizozichukua. Ni imani yetu kuwa wahusika watatekeleza maagizo hayo na kwamba tutafika mahali ambapo wakulima na wafugaji wataishi kwa kuheshimiana na kuthaminiana kwani kila kundi linamhitaji mwingine ili liweze kustawi,” alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles