Jeshi Sudan lazima jaribio la uasi

0
455
Vikosi vya Jeshi la Sudan vikirusha risasi hewani karibu na Makao Makuu na Ofisi za Usalama wa Taifa siku ya Jumanne

KHARTOUM, SUDAN

JESHI la Sudan limezima jaribio la uasi lililotekelezwa na kikosi maalumu cha usalama wa taifa ambacho awali kilikuwa kitiifu kwa rais aliyepinduliwa Omar al-Bashir, ripoti zinaeleza.

Mapambano yalianza Jumanne katika jiji la Khartoum ambapo milio ya milipuko ilisikika na kulazimisha uwanja wa ndege jijini humo kufungwa kwa muda.

Serikali inadai kuwa uasi huo umechochewa na malipo ya mafao, kitengo hicho cha usalama wa taifa kwa sasa kinavunjwa.

Wanajeshi wawili waliuawa na wengine wanne kujeruhiwa kwenye uasi huo.

Kiongozi mwandamizi wa baraza huru linaloongoza Sudan kwa sasa, Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, amemtuhumu Mkuu wa zamani wa Usalama wa Taifa, Salah Gosh kuchochea uasi huo.

Japo Dagalo anasema hachukulii jambo hilo kama jaribio la mapinduzi, lakini amesema jambo hilo halivumiliki.

Hadi kufikia jana asubuhi jeshi lilikuwa likiyashikilia makao makuu ya kikosi hicho.

Katika hotuba yake jana kiongozi wa baraza hilo, Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametangaza kuwa mapambano yameisha.

“Makao makuu yote yapo chini ya jeshi, na anga yetu imefunguliwa,” amesema.

Kiongozi wa baraza la mpito Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan amesema jeshi la nchi hiyo linaudhibiti wa majengo yote ya idara ya usalama wa taifa.

Katika hotuba yake  mapema jana kiongozi huyo aliapa kutoruhusu mapinduzi yoyote kutokea nchini humo.

Kumekuwa na wasiwasi juu ya uwezekao wa baadhi ya viongozi waliokuwa na ushawishi wakati wa Bashir kujaribu kutatiza mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo kwa hivi sasa.

Bashir ambaye alikaa madarakani kwa mkono wa chuma kwa miaka 30 alipinduliwa mwezi Aprili mwaka jana baada ya kuchachamaa kwa maandamano ya umma.

Mwezi Disemba mwaka jana alihukumiwa kifungo cha miaka miwili katika kituo cha kijamii.

Askari kutoka kitengo cha usalama wa taifa waliweka  mtandaoni picha za video zikionesha wenzao wakifyatua risasi hewani usiku kama alama ya uasi na kuonesha nguvu zao.

Shirika la habari la Reuters lmenukuu raia wakidai kuwa kulikuwa na mapambano katika wilaya ya kaskazini Khartoum, na jengo la usalama karibu na uwanja wa ndege kutekwa na waasi.

Vyanzo ndani ya jeshi vinaeleza kuwa vikosi vya serikali kwa sasa vimerejesha hali ya utulivu katika maeneo ambayo waasi walikuwa wakishambulia baada ya kufanya mazungumzo nao.

Kundi kubwa la waandamanaji wa nchi hiyo wametoa wito wa kukomeshwa kwa “oparesheni hizo zisokuwa na msingi ambazo zinawatia hofu wananchi.”

Mwaka jana wakati wa maandamano ya kumwondoa madarakani Rais Omar Al Bashir waandamanaji zaidi ya 170 waliuawa nchini Sudan, na kikosi hicho cha usalama wa taifa kililalamikiwa kutekeleza sehemu kubwa ya mauaji hayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here