27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Jeshi sasa kuanzisha benki

GRACE SHITUNDU NA ESTHER MNYIKA
CHAMA cha Akiba na Mikopo cha Ngome (Ngome Saccos) kinachoendeshwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ) kimewataka maofisa na askari kujiunga nao ili kufikia lengo la kuanzisha benki yao wenyewe itakayoitwa Ngome Benki.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Kanali Charo Yateri, wakati akitoa taarifa katika semina ya wakuu wa vikosi, vyuo na shule za mafunzo ya jeshi iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Blue Pearl.

Alisema benki hiyo ni moja ya miradi ambayo ipo katika mchakato wa kuanzishwa na chama hicho, lengo ni kuwasaidia wanajeshi kuweza kuweka na kukopa fedha zitakazowaletea maendeleo ya kiuchumi hata watakapostaafu.

“Tunatarajia benki iwe na mtaji wa Sh bilioni 50 (Authorised Share Capital) na kuuza hisa za Sh bilioni 20 (Issued Share Capital) wakati mtaji unaotakiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni kuanzia Sh bilioni 15,” alisema Kanali Yateri.

Alisema wanajeshi wengi wanahitaji mikopo, lakini changamoto iliyopo ni upungufu wa fedha, hivyo wanahitaji kuwa na wachangiaji wengi katika saccos hiyo ili wafikie malengo yote.

Alisema ni vizuri kuwawekea wanajeshi mazingira mazuri kabla ya kustaafu ili watakapomaliza kutumikia jeshi waweze kuwa na miradi na biashara mbalimbali zitakazowaingizia fedha za kujikimu.

“Tumewaita viongozi wa vikosi mbalimbali kuwapa elimu ya ujasiriamali ili nao waweze kuwaelimisha wafuasi wao umuhimu wa kujiunga na Saccos hii na maandalizi ya baadaye,” alisema.

Alisema wengi watastaafu na ni hatari kwa wanajeshi kuwa mtaani bila kuwa na shughuli itakayokuwa inawaingizia kipato, kwani wengine wanastaafu wakiwa na nguvu zao.

Awali akifungua semina hiyo, Brigedia Jenerali Ciril Mhaiki kwa niaba ya Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Meja Jenerali Salum Kijuu, alisema elimu ya ujasiriamali itawafaa askari na maofisa wote endapo wataitumia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles