25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jeshi lawalinda waandamanaji, al-Bashir agoma kung’atuka

KHARTOUM, SUDAN

WAKATI Rais Omar al-Bashir akiwagomea waandamanaji wanaomshinikiza ajiuzulu, jeshi la nchi hii limeingilia kati kuwalinda baada ya vikosi vya usalama kujaribu kuwaondoa kwa nguvu kutoka nje ya makao ya Wizara ya Ulinzi.

Wanajeshi walionekana wakijaribu kuyafukuza magari yaliyokuwa yakijaribu kurusha mabomu ya machozi katika siku ya pili ya maandamano ya kutaka Rais al- Bashir kung’atuka uongozini.

Waandamanaji walionekana wakitafuta hifadhi katika gari la jeshi la majini huku wasiwasi wa uwezekano wa makabiliano kati ya majeshi ukioonekana wazi.

Inavyoonekana waandamanaji wanatarajia mapinduzi, hivyo kuliomba jeshi kumtimua Bashir na kufungua njia ya kupatikana Serikali ya mpito.

Lakini Bashir amekataa kuondoka, akieleza kwamba wapinzani wake wanastahili kutafuta uongozi kupitia uchaguzi.

Wakiwa wameweka kambi katika makao hayo ya jeshi katikati ya mjini hapa, waandamanaji hawakujali kufyatuliwa mabomu ya machozi bali waliendelea kupaza sauti zao huku wakilitaka jeshi liwaunge mkono katika harakati zao.

Tangu maandamano hayo yalipoanza kote nchini hapa Desemba mwaka jana, maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, wale wa Idara ya Upelelezi na polisi wamekuwa wakiendelea kukamata watu wanaoandamana, lakini jeshi halikuwahi kufanya hivyo.

Waandamanaji tangu Jumamosi wameweka kambi karibu na makao makuu ya jeshi ambako pia ni makao ya Rais al- Bashir pamoja na Wizara ya Ulinzi.

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), askari wameweka vizuizi barabarani karibu na eneo hilo baada ya kushindwa kuwaondoa waandamanaji.

Waandamanaji wanaulalamikia utawala wa Rais al-Bashir kwa usimamizi mbaya wa uchumi jambo lililosababisha bei za vyakula kuongezeka pamoja na uhaba wa mara kwa mara wa mafuta na fedha za kigeni.

Serikali inakanusha madai hayo na badala yake inalaumu vikwazo vya Marekani kwa kusababisha matatizo ya kiuchumi nchini hapa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles