Khartoum, Sudan
Jeshi la Sudan limetangaza mafanikio makubwa baada ya kukomboa mji wa Wad Madani, mji muhimu mashariki mwa nchi hiyo, kutoka mikononi mwa vikosi vya wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF). Tukio hilo linaashiria hatua kubwa katika vita vya karibu miaka miwili kati ya pande hizo mbili.
Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha raia wakisherehekea barabarani huku wanajeshi wakiingia mji huo, ambao ni mji mkuu wa Jimbo la Al Jazira, umbali wa kilomita 140 kusini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
Kiongozi wa RSF, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo (maarufu kama Hemedti), amekiri kupitia ujumbe wa sauti kuwa vikosi vyake vilishindwa kukabiliana na mashambulizi ya angani yaliyotumia ndege zisizo na rubani zinazodaiwa kutengenezwa na Iran.
Hata hivyo, Hemedti ameapa kuendelea kupigana, akisema vita vinaweza kudumu hata kwa zaidi ya miaka 20, lakini hatarudi nyuma hadi ushindi upatikane.
Wad Madani ni mji wa kimkakati kutokana na nafasi yake kama kiungo muhimu cha usafirishaji na shughuli za kiuchumi kati ya Khartoum na maeneo ya kusini mwa Sudan. Mafanikio ya jeshi yanaweza kuwa na athari kubwa kwa mwelekeo wa vita hivyo vya muda mrefu.