Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Andrew Kundo amelitaka Jeshi la polisi nchini kufanya kazi kisasa ikiwa ni pamoja na kuwekeza kwenye teknolojia ili kupambana na uhalifu.
Kauli hiyo ameitoa Februari 21, 2022 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya usalama mtandaoni kwa wapelelezi na askari wa chumba cha mashtaka ambapo amesema kwa sasa maisha yamebadilika na yapo kwenye teknolojia hivyo ni lazima jeshi hilo lijipambanue kwa kuwekeza katika ufanyaji kazi kisasa.
“Sasa hivi tunaenda katika uchumi wa Kidigital ni lazima jeshi la polisi na lenyewe liende huko na endeleeni kuwekeza kwa vijana ili waone teknolojia ni muhimu na wataalamu wetu ni lazima wazidi kuongeza ujuzi ili kukabiliana na jambo hili,” amesema.
Aidha, amelitaka jeshi hilo kuona haja ya kuongeza ujuzi wa namna ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni ili kuwa na Jeshi la kisasa linalojibu kiu ya watanzania katika utekelezaji wa huduma bora.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi(SACP), Deusdedit Nsimeki, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yatawasaidia kupata uelewa wa masuala ya mtandao kwa kuhusisha makosa ya mtandao.