28.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 4, 2022

Jeshi kuunda serikali ya mpito ya miezi 18

BAMAKO, MALI

JESHI la mapinduzi nchini Mali limeapa kuunda serikali ya mpito ya muda wa miezi 18 ili kuirejesha nchi hiyo katika utawala wa kiraia baada ya mapinduzi ya mwezi uliopita dhidi ya serikali ya rais Ibrahim Boubacar Keita.

Kamati iliyoteuliwa na jeshi hilo la mapinduzi iliidhinisha kwa kauli moja “mkataba wa mpito” katika mkutano wa faragha kuhusu ubadilishanaji wa mamlaka hatua inayotoa njia kwa serikali ya muda itakayoongoza kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mpya.

Lakini moja ya masuala tata zaidi bado halijapata ufumbuzi kuhusu iwapo serikali hiyo ya mpito itaongozwa na raia ama mwanajeshi. Moussa Camara, katibu wa kamati hiyo, alisema jana kwamba serikali mpya itaundwa na wanachama zaidi ya 25, pamoja na waziri mkuu. 

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa chini ya mkataba wa awali, rais wala mawaziri wa serikali ya mpito hawawezi kuwania madaraka muda wao wa kuhudumu utakapokamilika.    

Camara alisema mashauriano ya siku tatu na viongozi wa kisiasa na makundi ya kiraia yaliunda mkataba wa mpito ambao pia utajumuisha makamu wa rais na baraza la mpito ambalo litahudumu kama bunge la taifa. Rais na Makamu wa rais watachaguliwa na kundi la watu watakaoteuliwa na uongozi wa jeshi.

Upinzani Mali, jamii za kimataifa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS wanamtaka kiongozi wa kiraia kuendesha kipindi cha mpito.

ECOWAS ambayo ina nchi 15 wanachama imeonya kuwa jeshi lazima limkabidhi madaraka kiongozi wa kiraia ifikapo wiki ijayo, au likabiliwe na vikwazo zaidi. Jumuiya hiyo tayari imesitisha uhamisho wowote wa kifedha nchini humo na imefunga mipaka yake na Mali.

Uongozi wa kijeshi, unaofahamika kama Kamati ya Kimataifa ya Ukombozi wa Watu, awali ilipendekeza miaka mitatu ya kipindi cha mpito ukisema kuwa katiba mpya lazima iandikwe kwanza. Soma zaidi: Hatua ya Jumuiya ya ECOWAS yakosolewa nchini Mali

Jumamosi, kiongozi wa kamati hiyo Kanali Assimi Goita, alisema anatumai watapata msaada wa kimataifa. “Ninajitolea mbele yenu kujitahidi kadri niwezavyo kuyatekeleza mapendekezo ya mashauriano haya ya siku tatu katika maslahi ya watu wa Mali,” alisema.

Baba Dakono, mtafiti na Taasisi ya Masomo ya Usalama ambaye anafuatilia kwa karibu mazungumzo hayo, alisema kama kiongozi wa kiraia atachaguliwa, watakuwa karibu na jeshi, na kutakuwa na uwepo mkubwa wa kijeshi katika nyadhifa nyingine zenye nguvu.

Alisema kuna uwezekano washiriki wengine wa kiraia watakuwa na mahusiano na muungano wa M5-RFP ambao ulifanya maandamano makubwa kwa wiki kadhaa kabla ya mapinduzi.

Nakala hiyo iliyoidhinishwa Jumamosi, inampa makamu wa rais udhibiti wa ulinzi, usalama na uanzishaji mpya wa serikali.

Shinikizo la kimataifa la kuwekwa haraka kipindi cha mpito linanuia kuepusha mgogoro wa kisiasa ambao huenda ukatumiwa na uasi wa itikadi kali. 

AFP

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,637FollowersFollow
545,000SubscribersSubscribe

Latest Articles