Na ASHA BANI – Dar es Salaam
SERIKALI imesema inatarajia kukamilisha ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), ifikapo Desemba.
Pia imesema pindi ujenzi utakapokamilika, uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuhudumia watu milioni sita kwa mwaka na ifikapo mwaka 2025 watafikia milioni 8.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, baada ya kumaliza kukagua jengo hilo linaloendelea kujengwa.
Profesa Mbarawa alisema ujenzi huo ambao umegharimu Sh bilioni 560, utasaidia kuondoa msongamano wa abiria kutoka eneo moja.
Alisema mradi wa uwanja huo awamu ya kwanza, ulianza Juni 2013 kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya HSBC na awamu ya pili inayoendelea itakamilika kwa fedha za ndani.
“Ukamilishaji wa jengo hilo utafanya kufikia viwanja 13 vinavyoendelea kukarabatiwa, ambavyo ni pamoja na Mwanza, Kilimanjaro, Songwe, Sumbawanga, Shinyanga, Kigoma na Tabora,” alisema.
Alisema kutokana na Serikali kufufua Shirika la Ndege (ATCL), imeona ni vyema kwenda sambamba na uboreshwaji wa viwanja vyake ili kuleta tija zaidi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JNIA, Salim Msangi, alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwa pamoja na malipo ya wakandarasi na kuchelewa kufika kwa vifaa vilivyokwamishwa bandarini.
“Kuchelewa kupatikana kwa fedha za kukamilisha mradi, ambapo Euro 121,634,888 hazijapatikana, Wizara ya Fedha na Mipango iliahidi kukamilisha taratibu za upatikanaji wa fedha hizo mapema ili kutoathiri utekelezaji wa mradi.
“Hadi kufikia Januari 19, mwaka huu, malipo ya hundi za Hazina (TVC) yalikuwa Sh bilioni 1.362 zinatakiwa ili kulipia vifaa vya ujenzi ambavyo vimekwama bandarini,” alisema.
Alisema kati ya fedha hizo, Sh milioni 960 zinazohitajika ni kwa kulipia vifaa maalumu vya usalama vya ukaguzi wa abiria (X-ray Machine), ambavyo vinahitaji kutoka haraka ili visiathiriwe na joto.
Akijibu hoja hiyo, Profesa Mbarawa alisema suala hilo tayari limepelekwa wizarani kwake na muda si mrefu vitalipiwa.