Na KENNETH NGELESI-MBEYA
SIKUKUU ya Mwaka Mpya imeanza kwa taharuki kwa wakazi wa Mtaa wa Soweto jijini Mbeya baada ya kuamka asubuhi na kukuta jeneza tupu likiwa limetelekezwa juu ya meza nje ya duka mtaani hapo.
Hatua hiyo iliwafanya wananchi wa eneo hilo kuanza kuitana huku wengine wakipigana vikumbo kwenda kushuhudia tukio hilo la kufungua mwaka mpya, ambalo linanasibishwa na imani za kishirikina.
Akizungumza na MTANZANIA jana jijini hapa, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Oscar Kilasi ambaye pia ni mfanyabiashara sokoni hapo, alisema kuwa alifika katika eneo hilo kufungua biashara mapema, lakini alipofika alijikuta akipigwa na butwaa baada ya kukuta jeneza lililotumika katika eneo hilo.
Alisema jeneza hilo lilikuwa limetelekezwa mbele ya duka lake, jambo ambalo lilimfanya ashangae na akalazimika kuwaita walinzi wa soko na kuanza kuwauliza kuhusu masahibu hayo.
“Nilipoliona jeneza likiwa juu ya meza nilimwita mlinzi ambaye nilimwona akiondoka kuingia ndani ya soko, nikamweleza na ndipo umati wa watu nao ukaanza kusogea kushuhudia tukio hili,” alisema Kilasi.
Naye mkazi wa Ilemi jijini hapa, Kefas Nkonde, alisema kuwa tukio hilo linatisha kwa vile si kitu cha kawaida jeneza kuonekana sokoni, na aliiomba Serikali ifanye uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo.
“Jeneza sio mzinga wa nyuki kwamba tutapenda kuungalia, bali ni kitu kinachoogopesha jamii, hivyo linapoonekana katika maeneo ambayo haikutarajiwa kuwepo ni vizuri Serikali ikafanya uchunguzi wa kina kujua kiini cha uwepo wake mahali hapa,” alisema Nkonde.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Soweto, Ramadhan Tavee, alisema kuwa tukio hilo limewashtua wananchi wa eneo hilo kwa kuwa si jambo la kawaida.
Alisema kuwa baada ya kuona tukio hilo, aliamua kuwasiliana na viongozi wake wa juu katika ngazi ya kata kabla hajapiga simu polisi kuomba msaada wa ulinzi.
“Nilipopata taarifa hii kama kiongozi nilifika mahali hapa mara moja kujiridhisha na niliona jeneza hili, niliwasiliana na viongozi wangu wa kata kisha nikapiga simu polisi na ninashukuru maana askari wamefika kwa wakati na kuhakikisha mtaa wangu unaendelea kuwa na amani na utulivu,” alisema Tavee.
Mwenyekiti wa Soko la Soweto, Fred Mwaiyongano alisema kuwa baada ya kuliona jeneza hilo, aliamua kufuatilia kwa kina ili kujua limefikaje sokoni hapo kwa sababu sio tukio la kawaida.
Alisema aliwasiliana na vijana wanaoshusha mizigo sokoni hapo ambao walimweleza kuwa jeneza hilo lilishushwa na gari aina ya Fuso lililokuwa limeleta nyanya likitokea Makambako mkoani Njombe.
“Pia tulipowasiliana na wapakiaji wa mizigo huko Njombe walisema jeneza hilo lilisafirisha mwili wa marehemu kutoka Mbeya kwenda Makambako na lilitakiwa kurudishwa Mbeya na ndipo wakalipakia kwenye Fuso hilo ili walipeleke kwenye msikiti mmojawapo uliopo Soko Matola Mbeya, lakini dereva akaliacha sokoni badala ya kulifikisha alikoelekezwa,” alisema Mwaiyonga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini sababu za jeneza hilo kutelekezwa sokoni hapo.
Kamanda Matei alisema kuwa mtu mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.