25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JENERALI ULIMWENGU ATOA SOMO ZITO

Lilian Justice Na Ashura Kazinja-MOROGORO


MWANAHABARI mkongwe, Jenerali Ulimwengu, amewataka waandishi wa habari na wahariri kufanya kazi bila woga licha ya kuwapo kwa changamoto kadhaa kwenye sekta ya habari nchini.

Alisema kwa zama za sasa, ni lazima kila mwanahabari atambue ana wajibu wa kulinda usalama wake na jamii anayoiandikia kwa kuzingatia misingi ya sheria.

Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa, alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Aliwataka wanahabari kufahamu kuwa sekta ya habari inapita kwenye changamoto nyingi ikiwamo kuibuka kwa vitisho na kupotezwa katika mazingira ya kutatanisha.

“Kwa zama hizi, ni lazima kutambua usalama wa mwandishi ni jambo la muhimu sana. Lakini pia tujiulize je, kuna uhuru wa uhariri katika vyumba vyetu vya habari na kama hilo halipo tujiulize kwanini?

“Suala la uhuru wa kujieleza katika kipindi cha miaka 25 iliyopita tuliweka misingi hiyo, lakini kwa sasa naona jambo hilo halipo tena.

“Ni wazi hata mtoto mchanga hatua ya kwanza baada ya kuzaliwa hulia, hiyo ni ishara tosha ya kwamba naye anahitaji haki zake za msingi ikiwemo kuishi,” alisema Ulimwengu.

Nguli huyo wa habari alisema kwa sasa taifa limekuwa likishuhudia matukio ya ajabu, ikiwamo kupotezwa kwa wanahabari, huku mamlaka za uchunguzi zikishindwa kutoa taarifa ya nini kinachoendelea.

“Hatari yenyewe kwa sasa mwandishi anapotezwa, jambo baya sana na mamlaka hazisemi, ni afadhali waseme kuwa tumempoteza mtu huyu kwa sababu hizi ili waliopo waweze kuchukua tahadhari. Vyumba vya habari, wahariri wote wamekuwa waoga hata linapotokea tukio la aina hii,” alisema.

Aidha Ulimwengu ambaye pia ni mwanasheria, alisema hali imekuwa mbaya, hususan baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Huduma kwa Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, ambayo alidai ni hatari kwa wanahabari.

Alisema sheria hiyo imempa mamlaka makubwa waziri mwenye dhamana kuwa ndiye mhariri wa taifa sambamba na kukimbilia kufungia, kukamata, kupiga faini na kumweka jela mwandishi.

“Sheria inaonekana wazi inambana mwandishi na hata kusababisha vyombo vya habari kufa kutokana na kukosekana kwa uhuru wa kujieleza na usalama wa mwandishi,” alisema Ulimwengu.

Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Kaimu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, alisema katika kipindi hiki vyombo vya habari vinapita katika kipindi kigumu kutokana na mabadiliko ya utandawazi.

“Pamoja na hili, leo wanahabari wanapotezwa, yuko wapi Azory Gwanda. Hivyo ndugu zangu tutumie mkutano huu kujadili hali ya tasnia ya habari nchini na tupate maoni ya namna gani tunatoka hapa tulipo,” alisema.

Licha ya hali hiyo, aliwataka wanahabari na wahariri kutambua jukumu lao kwa jamii la kuhabarisha, kuibua changamoto mbalimbali kwa masilahi ya taifa na watu wake.

“Leo tunapoingia kwenye vyumba vya habari, tunasema habari za siasa zinauza sana kuliko za kijamii, ndugu zangu hili si kweli, twendeni tutoe maelekezo kwa waandishi wetu wakaibue changamoto kwenye jamii, hasa za maji, elimu na afya pamoja na maeneo mengine,” alisema Balile

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles