33.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Jenerali Msuguri aadhimisha miaka 100 akiwa mkakamavu

Mwandishi Wetu – butiama

MKUU wa majeshi mstaafu, Jenerali David Msuguri, ameadhimisha miaka 100 tangu azaliwe Januari 4, 1920.

Licha ya uwezo wake wa kutembea kupungua, Jenerali Msuguri ambaye amelitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa miaka 55 na miezi saba, ameadhimisha miaka 100 akionekana mwenye nguvu tofauti na wengine wanaotimiza umri huo.

Mkuu huyo mstaafu wa majeshi aliadhimisha kumbukumbu hiyo jana nyumbani kwake Wilaya ya Butiama mkoani Mara kwa kufanya ibada ya misa takatifu iliyoongozwa na Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Musoma, Michela Msongazila.

Mwonekano wa Jenerali Msuguri mwenye nguvu na zaidi kufikisha umri mrefu, ulimlazimisha Askofu Msongazila  kuzungumzia siri hiyo, akisema kuwa inatokana na kuishi maisha ya nidhamu ya kijeshi na kumtukuza Mungu.

Akiwa ameketi kwenye kiti maalumu upande wa meza kuu, na zaidi akiwa ameambatana na familia yake, akiwamo mkewe Maria, Jenerali Msuguri alishiriki kikamilifu ibada hiyo iliyochukua saa kadhaa.

Tukio lililoibua gumzo na shangwe ni wakati kwaya ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Rwamkoma walipokuwa wakiimba ambapo Jenerali Msuguri aliwaomba wasaidizi wake kumsaidia kwenda walipo wanakwaya hao na kujumuika nao huku akionekana kuwa na bashasha.

Jenerali Msuguri ana historia ndefu na ya kipekee ndani na nje ya jeshi, akiwahi kushiriki vita ya pili ya dunia.

Lakini pia ndiye aliyeongoza ushindi wa  vita ya mwaka 1979 akiwa Mkuu wa Majeshi wa Tanzania kumwondoa Rais wa Uganda, Idd Amin Dada.

Akizungumza katika ibada ya maadhimisho ya Jenerali Msuguri kutimiza miaka 100, Askofu Msongazila amewataka Watanzania kudumisha amani na utulivu, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika Uchaguzi Mkuu.

MAMBO YANAYOPASWA KUZINGATIWA

Askofu Msongazila alisema yapo mambo ya muhimu ambayo Watanzania kwa umoja wao wanatakiwa kuzingatia ili kuhakikisha kunakuwa na amani na utulivu kwa miaka yote.

Alitaja mambo hayo kuwa ni pamoja na haki, kuheshimiana, kusikilizana, mazungumzo pamoja na kuvumiliana.

Aliongeza kuwa Watanzania wanapaswa kuhakikisha kuwa wanakuwa na woga mbele za Mwenyezi Mungu na maridhiano.

Askofu Msongazila alisema kuwa mambo yote haya yanapaswa kufanywa bila kujali umri, cheo, wadhifa au nafasi ya mtu katika jamii.

Alisema bila mambo hayo kuzingatiwa, amani na usalama wa nchi vitakuwa hatarini jambo ambalo asingependa litokee kutokana na misingi imara ya amani iliyojengwa na waasisi wa taifa hili.

KUWAENZI NA KUWALINDA WAZEE

Pia aliiomba Serikali kuwaenzi na kuwalinda wazee wote nchini kwa kuwapa huduma bora wanazostahili ili waweze kuishi vizuri.

Alisema wazee wametumikia nchi katika nafasi mbalimbali kijamii na kiserikali, hivyo ni vema wakapewa heshima wanayostahili, ambayo ni ulinzi na kuenziwa na Serikali ili nao waweze kuona umuhimu wao na mchango wao waliotoa katika jamii.

VIWANGO BIMA YA AFYA

Askofu Msongazila alisema katika suala la afya, Serikali inapaswa kuangalia upya viwango vya bima ya afya kwa maelezo kuwa gharama ziko juu kiasi kwamba wazee hao hawawezi kuzimudu.

Akitolea mfano viwango vya bima, alisema wazee wanatakiwa kulipia Sh 984,000 ili kuweza kupata huduma ya afya kiasi alichokitaja kuwa ni kikubwa kutokana na wengi wao kustaafu na watashindwa kumudu gharama hizo.

Alisema huduma ya afya ni miongoni mwa mambo muhimu kwa wazee, hivyo gharama inapokuwa kubwa kwa namna moja ama nyingine wengi wao watashindwa kumudu kutokana na ukweli kwamba hawana uwezo wa kuzalisha tena mali.

AWAASA VIJANA

Aidha Askofu Msongazila aliwaasa Watanzania hasa vijana kuwa na nidhamu ya maisha na kufanya mazoezi mbalimbali pia kuzingatia utaratibu wa ulaji wao ili waweze kuwa na maisha marefu zaidi.

NDOA NA MKE MMOJA KATI YA SITA

Kuhusu maisha ya kiimani ya Msuguri, Askofu Msongazila alisema takribani miaka mingi iliyopita alianza mchakato wa kurudi kanisani kwa kuandika barua.

Alisema pamoja na barua, pia alikuwa na mazungumzo naye ambapo baadaye aliamua kufunga ndoa na mke wake mmoja kati ya sita aliokuwa amewaoa kimila.

KAULI YA SERIKALI

 Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema Serikali inatambua mchango wa Jenerali Msuguri katika maendeleo ya nchi kwa ujumla, hivyo busara zake zitaendelea kutumika miaka yote.

Alisema kuwa kutokana na juhudi zake, Jenerali Msuguri aliwezesha Jeshi la Wananchi Tanzania kuwa miongoni mwa majeshi bora na yenye kuheshimiwa duniani na kuwataka Watanzania wengine kuiga mfano wake ili kutumikia nchi kwa moyo mmoja.

Malima alisema kuwa Jenerali Msuguri alijitolea maisha yake kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchi unakuwapo ambapo alifanikiwa kushinda kwenye vita ya Tanzania na Uganda aliyoiongoza.

ALICHOSEMA JENERALI MSUGURI

Akitoa shukrani katika hafla hiyo, Jenerali Msuguri aliwashukuru wote waliohudhuria hafla hiyo na kwamba yote yaliyozungumzwa na wasemaji ni ya kweli, huku akisisitiza kuwa yumkini alifanya zaidi ya hayo.

Alisema kuwa baada ya kustaafu jeshini ambako alitumika kwa miaka 55 na miezi saba, aliamua kurudi kijijini kwao Butiama ambako ndiko alikozaliwa na kwamba ndiko atakapozikwa mara atakapofariki dunia.

HUYU NDIYE MSUGURI

Taarifa fupi ambazo zinapatikana katika mitandao, zinamwelezea Jenerali David Msuguri kwamba alizaliwa Januari 4 mwaka 1920 huko Butiama mkoani Mara.

Mwaka 1942 Msuguri alijiunga katika vikosi vya jeshi la Mwingereza – King’s African Rifles (KAR) na baadae alifanya nao kazi nchini Madagascar.

Alianza kama ‘Private’ na mwaka 1957 utawala wa Uingereza ulianzisha cheo cha ‘effendi’ ndani ya KAR, walichopewa maofisa waandamizi wa kiafrika waliokuwa wakifanya vizuri ambapo Msuguri naye alipewa cheo hicho.

Desemba 1961, Tanganyika ikawa nchi huru na vikosi vya KAR vilihamishiwa katika vikosi vipya vya Jeshi la Tanganyika – Tanganyika Rifles.

Cheo cha ‘effendi kiliachwa muda mfupi baadaye na mwaka 1962 Msuguri akapandishwa cheo na kuwa Luteni.

Wakati wa maandamano ya Tanganyika Rifles ya Januari 1964, Msuguri alikuwa kituo cha Tabora.

Vikosi vya waasi vilivyojaribu kuondoa na kuchukua nafasi ya maofisa wao wa Kiingereza, walimtangaza Msuguri kuwa Meja.

Jenerali Msuguri alipanda vyeo na kufikia hadi kuwa katika nafasi ya Brigedia.

Mwaka 1979 alipandishwa cheo na kuwa Meja Jenerali na kuongoza JWTZ, na kukusanya vikosi kuvamia Uganda kufuatia kuzuka kwa Vita ya Uganda na Tanzania mwaka 1978.

Mwaka 1980 Msuguri aliteuliwa kuwa Mkuu wa JWTZ na Desemba 30 mwaka huo Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Julius Nyerere alimpandisha cheo na akawa Luteni Jenerali.

Februari 7, 1981 aliyekuwa Rais wa Uganda, Milton Obote alimpa Msuguri mikuki miwili kwa heshima ya ushindi wa vita.

Vita ambazo amepigana ni pamoja na vita ya pili ya dunia – World War II (Battle of Madagascar), Vita ya Kagera – Uganda – Tanzania War (Battle of Simba Hills, Battle of Masaka, Battle of Lukaya).

Alitangazwa kustaafu Agosti 31, 1988 na baada ya hapo alihamia Butiama mkoani Mara aliko hadi sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles