27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

JENERALI MABEYO, WATANZANIA WANAKUTEGEMEA KATIKA ULINZI WAO

NA PETER MITOLE,

FEBRUARI 2, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilitoa taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dk. John Pombe Magufuli amemteua aliyekuwa Luteni Jenerali Venance  Mabeyo kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi  Tanzania.

Luteni Jenerali Mabeyo ambaye baada ya uteuzi  amepandishwa cheo na kuwa Jenerali, amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Jenerali Davis Mwamunyange ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria.

Wahenga walisema: ‘‘Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni’’ Ni ukweli usiopingika Jenerali mstaafu  Mwamunyange katika utumishi wake wa kuliongoza Jeshi la Ulinzi kwa  muda wa takribani  miaka 10 baada ya kuteuliwa na Rais (mstaafu) Dk. Jakaya Kikwete Septemba 15,  2007, ameliacha Jeshi likiwa imara na mfano wa kuigwa kitaifa na kimataifa.

JWTZ limekuwa ni Jeshi lenye nidhamu ya hali ya juu si tu  kwa Amiri Jeshi Mkuu bali hata kwa wananchi wa kawaida  wanaowalinda.

Ni dhahiri Watanzania wamekuwa wakijivuna na kuona fahari kutokana na uwepo  wa jeshi lao madhubuti.  Imekuwa  kawaida mwanajeshi akipita mitaani utasikia wananchi wakisema:  ‘JW’ huyoo’ au ‘Mjeda wetu.’

Wananchi kulipenda jeshi lao kiasi hiki, si kwa ababu ya makombati yanayovaliwa na wanajeshi au umiliki wa zana kali  za kivita, bali ni matendo na uwajibikaji wa chombo hiki  wakati wa misukosuko na amani.

Wakati  Idd Amin wa Uganda amechokonoa mipaka yetu mwaka 1978, ni JWTZ kwa kushirikiana na vyombo vingine vya u Ulinzi na Usalama viliweza kumfurusha Nduli huyo.

Nchi yetu ikiingia  kwenye  migogoro ya kugombania mipaka na majirani zake kwa mfano mgongano uliopo kati yake na Malawi kuhusu Ziwa Nyasa,  JWTZ mara zote limekuwa likiwahakikishia Watanzania kuwa mipaka  iko salama na atakayethubutu kubipu atapigiwa kwani vocha zipo.

Ni Jeshi la Ulinzi  limefanya  bahari na maziwa kuwa salama baada ya  kuzuia vitendo hatari vikiwamo vya uvuvi haramu na mtandao wa uharamia unaochochewa na  machafuko ya kisiasa nchini Somalia.

Wakati wa amani jeshi hili limekuwa likijihusisha na kutoa misaada ya kunusuru uhai wa watu na mali zao  hasa pale inapojitokeza ajali kubwa au majanga ya asili  bila kusahau ujenzi wa miundombinu ya dharura panapojitokeza uharibifu wa ghafla.

Mwaka 2012, JWTZ kwa kushirikiana na majeshi mengine yalitoa  msaada wa dharura wa  matibabu kwa wananchi palipojitokeza  mgomo wa madaktari waliokuwa wakidai stahiki zao hususani Mkoa wa Dar es Salaam.

Kimataifa  Jeshi la Wananchi limekuwa likijichukulia sifa kemkem kwa kufanya shughuli zake kwa nidhamu na uadilifu  wa hali ya juu hasa pale linapokuwa linatoa ulinzi katika nchi zenye mizozo.

Jenerali Venance Mabeyo unapopokea kijiti cha uongozi kutoka kwa mtangulizi wako, huna budi kuendelea kuliboresha  jeshi ili liendelee kuwa kimbilio ndani na nje hasa katika wakati huu dunia inapokabiliwa na matukio ya ugaidi na ukiukwaji mkubwa  wa haki za binadamu.

 Si dhambi katika zama hizi za Sayansi na Teknolojia,  Jenerali Mabeyo kuliwezesha jeshi kuwa na wasomi maprofesa wanaoweza kufanya tafiti mbalimbali ili kuibuka na mbinu mpya za kivita na kufahamu namna ya kutatua migogoro ya kisiasa, kiuchumi kijamii na kisayansi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles