Ahmed Makongo -Bunda
MAHAKAMA ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara, imemhukumu kifungo cha maisha jela Masatu Mjarifu (35), baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka mitatu.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mwandami wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Jackline Rugemalila, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka pasipokuacha shaka.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka wa Serikali Inspekta wa Polisi, Theophil Mazuge, kuwa Desema 26 mwaka 2018 majira ya saa mbili asubuhi, mshtakiwa ambaye ni mvuvi na mkazi wa Kijiji cha Mahyolo wilayani Bunda, aliondoka nyumbani kwake na kwenda nyumbani kwa jirani yake.
Inspekta Mazuge alidai kuwa ya kufika nyumbani hapo kwa jirani yake, alimchukua mtoto huyo na kuingia naye kwenye chumba chake na kuanza kumbaka.
Alidai mama wa mtoto huyo aliporejea nyumbani hakumuona mwanaye na ndipo alipoanza kumtafuta, ambapo alifanikiwa kumkuta nyumbani kwa mshitakiwa akibakwa na mwanaume huyo na ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada na wananchi wakafika katika eneo la tukio.
Alidai kuwa mshitakiwa huyo alijaribu kutoroka lakini alikamatwa na kupelekwa polisi katika kituo kidogo cha Kibara na ndipo kesi namba 168 ya mwaka 2019 ilipofunguliwa, ambapo katika kuthibitisha shitaka hilo upande wa jamhuri uliita mashahidi wanne huku mshitakiwa akijitetea mwenyewe.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, mshitakiwa alipewa fursa ya kujitetea na kuiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa nimkosaji wa mara ya kwanza.
Hata hivyo Inspekta Mazuge aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa, ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye nia au tabia hiyo, kwani vitendo vya ubakaji vinaonekana kuzoeleka ndani ya jamii na watu kuviona ni vya kawaida.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Rugemalila alimuhukumu mshitakiwa kifungo cha maisha jela.