Na Malima Lubasha, Serengeti
Mahakama ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara imemhukumu, Yusufu Chacha(22) mkazi wa kijiji cha Nyansurura kwenda jela miaka mitatu na kulipa faini ya Sh milioni 1 baada ya kukutwa na hatia ya kumpiga na jiwe na kumsababishia upofu mwanafunzi wa kidato cha nne, Esther Chacha(18).
Hukumu hiyo imetolewa jana Juni 30, mwaka huu na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Judith Semkiwa, baada ya kujiridhisha na hoja za ushahidi zilizowasilishwa mahakamani hapo pasi na shaka.
“Mahakama baada ya kuzingatia maelezo ya pande zote mbili bila kuacha shaka yoyote inakuhukumu kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela pamoja na kulipa faini Sh milioni 1 kwa kosa la kumpiga jiwe na kumsababishia upofu wa jicho la kushoto, Esther Chache(18) mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya Sekondari ya Nyansurura,” amesema Hakimu Semkiwa.
Upande wa Mashtaka ukiongozwa na Mwendesha Mashtaka, Faru Maengela ulikuwa na mashahidi sita akiwemo mlalamikaji huku upande wa mlalamikiwa ukiwa na mashahidi watatu ambapo kati yao mmoja alikataa kutoa ushahidi wake kwa kile alichoeleza kuwa mazingira ya kosa hayafahamu vizuri.
Aidha, upande wa mshtakiwa mmoja wa mashahidi ulitoa ushahidi ambao ulitofautiana na kwa maelezo kuwa hata jina la mshtakiwa halijui huku shahidi wa pili alidai kuwa siku ya tukio yeye alikuwa nyumbani kwake na familia na kwamba alishanga kuitwa mahakamani kutoa ushahidi.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, katika kesi hiyo ya jinai namba 48 ya mwaka 2021, Yusufu Chacha(22) Novemba 1, 2020 akiwa katika sherehe ya mahafali ya kidato cha nne katika kijiji cha Nyansurura alimpiga na jiwe, Esther Chacha katika jicho lake la kushoto na kuanguka chini alipokuwa akicheza muziki.