27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Jecha wa ZEC achomoka mafichoni

mtz1.jpg..*Dk. Shein asisitiza uchaguzi utafanyika Z’bar

Jonas Mushi na Esther Mnyika, Dar es Salaam

HATIMAYE Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, jana ameonekana hadharani katika maadhimisho ya sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi zilizofanyika kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja.

Jecha ambaye inaaminika alikuwa mafichoni tangu alipotangaza kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka jana, alionekana ameketi kwenye jukwaa kuu la viongozi, jirani na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Kuonekana kwa Jecha hadharani kumezua mijadala mitaani na hata katika mitandao ya kijamii, huku wengi wakihoji alikuwa wapi mara baada ya kufuta matokeo ya uchaguzi.

Watu mbalimbali wamekuwa wakihoji kuonekana kwa Jecha hadharani jana, siku ambayo Dk. Shein alitumia maadhimisho ya Mapinduzi kutangaza kwamba uchaguzi wa marudio Zanzibar iwe isiwe utafanyika.

Oktoba 28, mwaka jana majira ya saa sita mchana kwenye Ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar zilizopo Kilimani mjini Unguja, ilikuwa ndiyo siku ya mwisho kuonekana Jecha hadharani.

Siku hiyo huku akiwa chini ya ulinzi wa vijana wawili wanaoaminika kuwa ni makomandoo wa Jeshi la Ulinzi wa Tanzania (JWTZ) waliovaa kiraia, Jecha alitangaza kuufuta uchaguzi wa Zanzibar mbele ya vyombo vichache vya habari.

Alitumia dakika mbili tu kuvitangazia vyombo hivyo vya habari juu ya adhima yake ya kuufuta uchaguzi na kutoa sababu zilizomfanya kufanya hivyo ikiwamo kuharibiwa kwa uchaguzi kisiwani Pemba.

Hata hivyo, baada ya kumaliza kutoa taarifa yake kwa vyombo hivyo, Jecha hakutaka kuulizwa maswali.

Oktoba 27, mwaka jana ikiwa ni siku moja kabla ya kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi, Jecha pia hakuonekana kwenye kituo cha kutangaza matokeo kilichokuwa katika Hoteli ya Bwawani kwa kile kilichodaiwa alipata matatizo ya kiafya na hivyo kumwachia kazi hiyo Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Abdulhakim Ameir Issa.

Siku hiyo majira ya saa kumi jioni, askari wa JWTZ walizingira kituo cha Bwawani na kuwaamuru watu waliokuwa ndani kutotoka nje na hata wale walioko nje ya kituo hicho kutosogea.

Watu waliokuwa ndani ya kituo hicho wengi wao walikuwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi pamoja na baadhi ya wawakilishi wa vyama vya siasa waliofika kusikiliza matokeo ya uchaguzi.

 

  1. SHEIN NA UCHAGUZI

Kutokana na kile kinachoonekana kuendelea kupasuka kwa hali ya kisiasa visiwani Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema uchaguzi utarudiwa baada ya awali matokeo yake kufutwa na ZEC.

Kauli hiyo ya Dk. Shein inakuja siku moja baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ambaye alikuwa mgombea urais kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kueleza msimamo wake wa kutokubali kurudiwa kwa uchaguzi visiwani humo na badala yake akitaka aliyeshinda atangazwe kwa kuheshimu maamuzi ya wananchi waliyofanya Oktoba 25, mwaka jana.

Akihutubia katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Uwanja wa Amaan jana, Dk. Shein alisema uchaguzi huo utarudiwa kwa mujibu wa katiba na sheria.

“Kila mmoja anajua kilichotokea katika uchaguzi Zanzibar baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi kutokana na kasoro zilizogundulika kutokea wakati wa uchaguzi huo,” alisema Dk. Shein na kuongeza:

“Suala la kurudiwa kwa uchaguzi liko palepale na utarudiwa kwa mujibu wa katiba na sheria, hivyo nawaomba wananchi muwe na uvumilivu na upendo wakati tukisubiri kutangazwa kwa tarehe ya kurudiwa uchaguzi.”

Licha ya kwamba kila upande umeshaweka msimamo wake, lakini Dk. Shein alisema mazungumzo ya kusaka suluhu yanaendelea baina ya pande hizo na kwamba taarifa ya mazungumzo hayo itatolewa punde yatakapokamilika.

“Tangu kutokea kwa mgogoro huu tulishauriana kukutana viongozi sita waliopo madarakani na waliostaafu ili kufanya mazungumzo ya kusaka suluhu na taarifa itatolewa pindi mazungumzo yatakapokamilika,” alisema Dk. Shein.

 

BALOZI SEIF NA VIJEMBE

Awali akisoma hotuba ya kumkaribisha mgeni rasmi, Makamu wa Kwanza wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, alirusha kijembe kwa viongozi wa Serikali ambao wamesusia sherehe hizo.

Alisema hatua ya kutoshiriki kwao isingeweza kukwamisha sherehe hizo za Mapinduzi.

“Nawashukuru sana viongozi na wananchi mliofika hapa kufanikisha sherehe hizi na wengine wale ambao hawajaja walifikiri tungeshindwa kuadhimisha sherehe hizi, lakini tumefanikiwa,” alisema Balozi Iddi.

Kutoonekana kwa Maalim Seif katika sherehe hizo ni mwendelezo wa msimamo wa CUF wa kutoshiriki shughuli zozote za Serikali, huku wakitaka matokeo ya uchaguzi yatangazwe.

Januari 3, mwaka huu Chama cha Wananchi (CUF), kilitangaza kutoshiriki katika shughuli za wiki ya maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi Zanzibar zinazoadhimishwa Januari 12 ya kila mwaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles