Na William Shao,
Ulaji wa nyama nyekundu unaweza kuongeza hatari ya figo zako kushindwa kufanya kazi, hiyo ni kwa mujibu wa utafiti mpya unaopendekeza watu kula vyakula vingine vyenye protini kama samaki na mayai ambavyo vinaweza kupunguza hatari hiyo na kuacha kula nyama nyekundu.
Idadi inayoongezeka ya watu mmoja mmoja sasa inazidi kuwa na magonjwa sugu ya figo (chronic kidney disease—CKD) kutokana na mazoea ya kula nyama nyekundu), na wengi wao huendelea hivyo hadi kufikia hatua hatari ya maradhi hayo inayojulikana kama ESRD (end-stage renal disease), wanasema watafiti katika Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Kisukari, Utumbo na Figo (NIH) iliyoki Maryland, Marekani.
Hatua hiyo, ESRD, huhitaji usafishaji damu kwa mashine ya figo (dialysis) au hata kufanyiwa upasuaji na kupandikizwa figo nyingine.
Kwa mujibu wa ‘The Economic Times’ la India la Julai 16, 2016, mwongozo wa sasa wa tiba unapendekeza watu kujizuia kula vyakula vyenye protini nyingi ili kuzuia au kudhibiti CKD na kuzuia maradhi hayo yasifike kwenye hatua ya ESRD.
Katika kuchunguza uhusiano ulioko kati ya kula nyama nyekundu na maradhi ya figo, watafiti katika Chuo cha Tiba cha Duke-NUS na Chuo Kikuu cha Singapore walichambua data kutoka katika tafiti zilizofanywa na watafiti wa tiba wa China juu ya Wachina, watu wazima 63,257. Uchambuzi huo ulifanyika nchini Singapore.
Katika utafiti uliochapishwa katika jarida ‘American Society of Nephrology’, ilielezwa kuwa watu hao 63,257 ni idadi ambako asilimia 97 ya nyama nyekundu huliwa. Idadi hiyo ilipofuatiliwa kwa wastani wa miaka 15, watafiti waligundua kuwa ulaji wa nyama nyekundu ulihusika moja kwa moja na maradhi ya figo.