WIKI iliyopita tuliishia namba mbili katika maelezo ya vipimo muhimu vitakavyokufanya ujue kama uzito wako hauhusiani na dalili za TOFI.
Leo tunaendelea kwa kuangalia namba tatu:
3. Angalia kiwango cha viondoa cholestro mwilini mwako (High density Lipoprotein).
Kiwango hiki kinatakiwa kiwe zaidi ya 60mg/dl
4. Angalia kiwango cha triglycerides( mafuta mabaya yanayo hifadhiwa mwilini baada ya sukari kuzidi kiwango maalumu).
Kiwango hiki kiwe chini ya 100mg kwa kuwa kikiwa zaidi ya hapo unakuwa hatarini kupata magonjwa sugu bila kujali una uzito kiasi gani na wenye afya.
5. Pima shinikizo la damu kwani ni kipimo kizuri kinaweza kukuambia na kukupa ishara kama unakiuka ulaji sahihi.
6. Pima kiwango cha homoni za tezi ya thyroid kama thyroxine -T4 na Tri iodothyronine -T3 kwani vinapokuwa katika kiwango cha juu pia vinaweza kusababisha uzito wako kuwa chini ya kiwango na dalili zinginezo kama kutohimili joto, kudhoofika na mapigo ya moyo kwenda kasi.
Kwa maelezo hapo juu, ni ishara kwamba pale unapokuwa unajenga fikra kwamba kwa sababu wewe una uzito wenye kilo nzuri kiafya, basi magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu hutaweza kuyapata, utakuwa unazidi kuyaangamiza maisha yako kwa kudhoofisha afya yako kutokana na kutobadili mwenendo wako wa lishe.
Vipimo vyote hivyo unaweza kuvipata katika hospitali yoyote kubwa.
Kuna baadhi ya watu kwa sababu tu wana uzito mdogo kimwonekano, basi huendelea kutumia vyakula vyenye sukari nyingi, wanga kwa wingi, vyenye vionjo vingi vya kemikali na unywaji wa juisi zenye kuongeza nguvu zenye sukari nyingi, hii hali inafanya mwili wako kuendelea kurundika mafuta katika ogani za mwili ndani kama ini na figo.
Hivyo basi, njia pekee ya kujijengea uzito wenye afya ni kufanya mambo yafuatayo; kama tayari umeonekana una kilo za kawaida lakini una vipimo vyenye kasoro, hizi ni mbinu chache za kutibu tatizo lako haraka kwa kupata lishe bora.
1. Epuka au punguza vyakula vyenye wanga nyingi na sukari nyingi, kama wali, ugali, mikate, chapati na vyakula vingine vya ngano, tambi, viazi vitamu na mviringo.
2. Epuka matumizi ya vinywaji vilivyo ongezewa sukari, rangi na kemikali za vionjo mbalimbali.
3. Epuka matumizi ya juisi za matunda yenye sukari nyingi, tumia matunda kama zabibu, parachichi na stroberi, kwa kuwa  ni miongoni mwa matunda yenye sukari kidogo.
4. Tumia Vyakula vya fats kwa wingi kama olive oil, alizeti, karanga, nyama za mifugo yote inayokula nyasi, samaki, mayai na kiini chake (kienyeji) na nazi. Hapa utaufanya mwili wako ujijengee mazingira ya kutumia mafuta au ketone bodies badala ya glucosi na kuufanya mwili wako kuwa wenye nguvu, lishe hii inaonesha kushusha kolestro mbaya na kuongeza utandaji kazi wa mwili. Watu wengi wamekuwa wakishukuru kwa kuwa inawasaidia kutibu magonjwa mengi.
5. Tumia vyakula vya protini kwa wastani kwani endapo ukitumia kiwango kikubwa mwili wako utaanza kubadili protini kuwa sukari kupitia Gluconeogenesis. Vyakula hivi ni kama nyama, karanga, ufuta, samaki, mayai na parachichi.
Itaendelea wiki ijayo…