Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Katika kuhakikisha wanafunzi walioko vyuoni nchini wanazitambua fursa mbalimbali katika kilimo, viwanda na masoko na kuzitumia fursa hizo kujiajiri na kujipatia kipato, kampuni ya Jatu Plc kupitia viongozi wake wamezungumza na wanafunzi Chuo cha Uhasibu(TIA) yenye nia ya kuwawezesha vijana hao kufikia adhma hiyo.
Kampuni ya Jatu imeanza rasmi mazungumzo hayo na wanafunzi kupitia progamu yao iitwayo JATU UNITALK inayoongozwa na balozi wa Jatu ambaye pia ni Mlimbwende wa Tanzania kwa mwaka 2018, Queenelizabeth Mukane.
Awali akizungumza na wanafunzi wa chuo hicho Mlimbwende Queen alisema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu kwa wanafunzi walioko vyuoni na kuziainiasha fursa za uwekezaji zilizopo ndani ya kampuni hiyo na kuzigeuza katika uhalisia hali ambayo itachangia
kuongeza fursa za kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.
Naye, Meneja Mkuu wa Jatu, Mohammed Simbano, akizungumza na wanafunzi wa Chuo hicho, alisema kuwa, ndani ya kampuni hiyo kuna fursa nyingi ambazo kila kijana akizitumia ipasavyo zinaweza kuwa na tija kwake na jamii kwa ujumla.
Aidha, Simbano alisema kwamba; “Chini ya program hiyo ya JATU UNITALK lengo kubwa ni kumpatia kijana wa kitanzania fursa zilizopo katika sekta ya uwekezaji na kutambua njia sahihi za kufanikisha malengo hayo kutokana na programu hiyo kutoa mbinu za kutosha kuhusu uwekezaji,” amesema.
Pamoja na hayo, Mkuu wa Idara ya Masoko, Mary Chulle aliwaeleza wanafunzi hao kuhusu namna wanavyoweza kujitengenezea kipato kupitia masoko ya bidhaa za Jatu pindi wanapofanya manunuzi ya bidhaa za chakula.
Akieleza kuhusu fursa hiyo, Chulle alisema kuwa ndani ya Jatu chakula pia ni fursa na humuwezesha mtumiaji kupata gawio la faida la asilimia 10 kwa kila manunuzi anayofanya kupitia mfumo wa Jatu Masoko.
Mbali na hayo, akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa chuo hicho, rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo hicho, Stanslaus Kisinza, alisema kupitia program hiyo ya Jatu itaenda kusaidia wanafunzi wengi wa vyuo nchini kupata ujuzi wa kutosha katika nyanja mbalimbali hususani katika kilimo, viwanda, masoko na sekta ya uwekezaji kwa ujumla kama ilivyo adhama na dira ya kampuni ya Jatu.
Kwa upande wake, Balozi wa Jatu Unitalk Mlimbwende Queen Elizabeth Mukame pamoja na mambo mengine aliwataka wanafunzi hao kuitumia elimu kwa vitendo ili kuwa na utayari wa kujiinua kiuchumi na hivyo kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo.
Mbali na hayo, Mlimbwende huyo alisema kuwa, zipo faida nyingi ambazo wanafunzi watazipata kupitia programu hiyo ya Jatu Unitalk ikiwa ni pamoja na kuwapa uelewa mzuri wanafunzi wa vyuo kuhusu mbinu za kujiunga na masoko ya mitaji na uwekezaji chini ya taasisi ya Jatu.
Itakumbukwa kwamba , Program ya JATU UNITALK ilizinduliwa rasmi mwanzoni mwa mwezi Januari, huku ikilenga kutoa elimu kwa wanafunzi waliopo katika vyuo mbalimbali nchini na kuwawezesha kupambana na soko la ajira kwa kujiajiri wenyewe kupitia uwekezaji wenye tija.