26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

January: Tukimaliza mifuko ya plastiki tutachukua hatua nyingine

Na ELIZABETH HOMBO

-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, amesema utekelezaji matumizi ya mifuko mbadala utakapokamilika baada ya mwaka mmoja watafanya tathmini na kuchukua hatua nyingine.

January ambaye jana alitumia muda mwingi kutembelea maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kufuatilia utekelezaji marufuku mifuko ya plastiki, alitoa kauli hiyo baada ya gazeti hili kutaka kufahamu iwapo Tanzania itachukua hatua kupiga marufuku bidhaa nyingine za plastiki, kama mirija, sahani na nyinginezo kama ilivyofanywa na Bunge la Umoja wa Ulaya.

Katika hilo, January alisema itakapofanyika tathmini baada ya mwaka mmoja, wataangalia hatua nyingine.

Bunge la Umoja wa Ulaya tayari limepitisha azimio la kupiga marufuku bidhaa za plastiki kama mifuko, mirija, sahani, vijiti vya pamba vya kusafishia masikio na nyingine ifikapo mwaka 2021.

Tanzania kama ilivyo nchi nyingine duniani, inatekeleza azimio la Umoja wa Mataifa linalotaka dunia kuteketeza bidhaa za plastiki, ikiwamo mifuko ambayo inaonekana kuathiri viumbe hai.

Tayari nchi 127 duniani zimechukua hatua kati ya 192, huku UN ikieleza kuwa marufuku hiyo ya mifuko ya plastiki ni asilimia 40 tu ya taka ambazo dunia inapaswa kuziteketeza.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana baada ya kuhutubia wananchi katika viwanja vya Zakhem Mbagala, Dar es Salaam, January alisema; 

“Tutakwenda hatua kwa hatua, kuhusu azimio hilo la Umoja wa Ulaya kwa sasa ni mapema, tutaenda hatua kwa hatua na hatuwezi kufanya yote kwa pamoja. 

“Pia tutaangalia bidhaa yenye mbadala kwa urahisi ndiyo tutaanza na hilo, lakini hatuwezi kufanya yote kwa pamoja,” alisema January.

Awali akiwahutubia wananchi hao, January alisema maeneo aliyozunguka kukagua siku ya kwanza ya matumizi ya mifuko mbadala, ikiwemo Kariakoo amegundua bado kuna kazi ya kuelimisha watu.

Kutokana na hilo, aliwataka watendaji wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kurudi Kariakoo na kupita maeneo yote ya Dar es Salaam, kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu matumizi ya mifuko mbadala.

“Sasa kesho (leo) NEMC hakutakuwa na ‘off’ (mapumziko) muendelee na zoezi, mpite kila sehemu na kujibu maswali yote, kwa sababu kwa namna nilivyokuwa naulizwa maswali bado kuna changamoto,” alisema January.

Aidha, alisema tayari kuna makontena yenye mifuko mbadala yako kwenye meli yanakuja nchini na baada ya mwezi mmoja yatakuwa yamefika.

Aliwatoa hofu wananchi kwamba baada ya mifuko hiyo mbadala kuwasili nchini, bei ya bidhaa hiyo itakuwa imeshuka.

“Pia nimefarijika Watanzania wameonyesha umakini na niwatoe hofu kuwa baada ya makontena kuwasili bei itakuwa imeshuka,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, alisema tayari kampuni tano zimejitokeza zikitaka kuchukua mifuko ya plastiki kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo ndoo.

“Zoezi hili limewafikia wengi na tayari kampuni tano zimejitokeza kuchukua mifuko hiyo, ikiwemo kiwanda cha sementi ambao wanahitaji kwa ajili ya kutumia kama chanzo cha nishati,” alisema Dk. Gwamaka.

Akizungumzia kuhusu vifungashio vilivyoruhusiwa baada ya kutumiwa kama vinafaa kubebea bidhaa nyingine, mwanasheria wa NEMC, Manchare Heche alisema ni marufuku.

“Hairuhusiwi kabisa kutumia vifungashio ambavyo vilitumika kwa ajili ya bidhaa fulani kama sukari, mkate nk… vifungashio ni ‘special’ (maalumu) kwa ajili ya bidhaa iliyofungiwa,” alisema Heche.

MWITIKIO 

Ikiwa jana ilikuwa mwanzo wa matumizi ya mbadala wa mifuko ya plastiki, MTANZANIA Jumapili lilizunguka katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, hasa yenye wafanyabiashara na kushuhudia namna wananchi wengi walivyozingatia katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki.

Katika maeneo hayo, wanawake wengi walionekana wamebeba vikapu kuwekea mahitaji yao.  

Katika maeneo ya maduka ya kuuzia nyama, watu wengi walionekana wakiwa wamebeba ama mifuko ya karatasi au ndoo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles