27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

JANUARY KUUNDA KIKOSI KAZI KULIOKOA ZIWA JIPE

Na DENNIS LUAMBANO, MWANGA


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, amesema ataunda kikosi kazi kitakachosaidia kuliokoa Ziwa Jipe, ambalo liko hatarini kutoweka baada ya magugu maji kuota katika eneo kubwa la ziwa hilo kwa upande wa Tanzania.

Aliwataja maofisa wataalamu watakaounda kikosi hicho kuwa ni kutoka wizara yake, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.

January alitoa kauli hiyo mjini hapa juzi, baada ya kulitembelea na kufanya mkutano wa hadhara na wakazi wa Kijiji cha Butu Ugweno, Kata ya Jipe, wilayani Mwanga, wanaoishi karibu na ziwa hilo.

January yuko katika ziara ya kukagua shughuli za uhifadhi wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.

"Ziwa Jipe ambalo liko Tanzania na Kenya, liko hatarini kupotea kutokana na shughuli za kiuchumi zinazoendelea kufanywa katika maeneo ya karibu yanayolizunguka, ikiwamo uvuvi.

"Kutokana na hali inavyoendelea, ziwa hili litapotea kabisa na hatutakuwa na ziwa kabisa, sisi Serikali hatukubali hali hii itokee.

"Lazima tulilinde na tunavyotaka kuliokoa si jambo letu serikalini, bali ni jambo la mazingira na jambo la kijamii. Kwa sababu hifadhi ya mazingira si jambo dogo na tutasaidia katika kulihifadhi na tutaunda kikosi kazi ili tupange mpango wa pamoja wa kuliokoa.

“Si hivyo tu, pia tutalitangaza katika Gazeti la Serikali ili kuwe na masharti ya ziada ya matumizi yake na litakuwa ni eneo la mazingira linalolindwa,” alisema January.

Aliendelea kusema kuwa, baada ya masharti hayo kutakuwa na kipindi cha mpito na Serikali itakuwa makini ili mazingira yote yanayolizunguka ziwa hilo kwa upande wa Tanzania, yasiendelee kuharibiwa.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aron Mbohogo, alisema wao walishaanza kuwazuia watu wasiendelee kuharibu mazingira ya ziwa hilo, ingawa walikuwa hawajui wanatumia vifungu gani vya sheria.

Alisema uamuzi alioutoa January utawaongezea nguvu ya kulilinda ziwa hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles