23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JANUARY ATAJA KERO SUGU ZA MUUNGANO

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba

 

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, amezitaja kero tatu za Muungano zisizotatuliwa hadi sasa.

Kero hizo alizitaja mjini hapa jana akiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenister Mhagama na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, yatakayofanyika wiki ijayo.

Alizitaja kero hizo kuwa ni usajili wa vyombo vya moto kutumika Zanzibar na Tanzania Bara, hisa za Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na mapendekezo ya tume ya pamoja ya fedha kuhusu mgawanyo wa mapato ya Muungano na utaratibu wa kuchangia gharama za Muungano.

January alisema, Serikali imejitahidi kutatua kero za Muungano ambapo kwa sasa zimebaki hizo tatu tu kati ya 15.

Alisema kero hizo zinaendelea kujadiliwa jinsi ya kuzitatua, huku ile ya usajili wa vyombo vya moto akisema kinachosubiriwa ni kupitishwa kwa sheria ya usalama barabarani.

“Suala la kero ya usajii wa vyombo vya moto linamalizwa kwa utaratibu wa kisheria, sheria ipo katika mchakato wa kutungwa, imani yetu sheria imeanza na waraka upo litakwisha mapema,’’ alisema.

Pia alisema kero nyingine ni hisa za Zanzibar katika iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na alisisitiza kuwa nayo itatatuliwa.

“Tutakumbuka kabla ya Muungano nchi zetu hizi, ikiwamo Zanzibar kama dola ilikuwa kama mjumbe wa sarafu wa Afrika Mashariki tulipounda Benki Kuu ya Tanzania, hisa zile zikahamishwa kwa Benki Kuu. Kwa hiyo upo mjadala wa kuweza kutambua hisa hizo na gawio la Zanzibar kwa faida inayopatikana katika biashara ya Benki Kuu, hilo linashughulikiwa na linakaribia kumalizika kwa sababu nyaraka zipo,’’ alisema.

Kuhusu kero ya mapendekezo ya tume ya pamoja ya fedha kuhusu mgawanyo wa mapato ya Muungano na utaratibu wa kuchangia gharama za Muungano, alisema yanangoja uamuzi wa Serikali na utafikiwa hivi karibuni.

“Hizi kero si za kupasua Muungano na tayari yanafanyiwa kazi na katika kikao cha pamoja kitakuwa na ripoti juu ya utekelezaji wa hayo,’’ alisema.

Kwa upande wake, Jenister alisema maadhimisho ya Muungano yanatarajiwa kufanyika Dodoma na Rais Dk. John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

“Shughuli zitakazofanywa katika maadhimisho hayo ni gwaride la heshima lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama, maonesho ya kikosi cha makomandoo, onyesho la farasi na mbwa waliofunzwa, onesho la ukakamavu kwa wanafunzi wa sekondari,’’ alisema.

Naye Rugimbana aliwataka wakazi wa mikoa ya jirani na Dodoma kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Jamhuri.

Alisema kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho hayo ni tuulinde na kuuimarisha Muungano, tupige vita dawa za kulevya na kufanya kazi kwa bidii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles