Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa jimbo la Bumbuli Mkoani Tanga Januari Makamba amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua katika kipindi chake kuwa Waziri wa Nishati na Mambo ya Nje na kusema jambo hilo litaendelea kuwa historia isiyofutika katika maisha yake.
Akizungumza leo Februari 24, 2025 katika mkutano wa hadhara ulifanyika viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Lushoto, Tanga, amesema amejifunza mengi kupitia uongozi wake.
“Mheshimiwa Rais, naomba nikushukuru sana kutoka sakafu ya moyo wangu kwa kuniamini mimi kuniteua waziri wako, kwanza wa nishati na baadaye Mambo ya Nje ni heshima kubwa ambayo haitafutika katika uhai wa maisha yangu.
“Katika kipindi ambacho nimefanya kazi na wewe nimejifunza sana na nimeerevuka kutokana na uongozi wako. Lakini nimeerevuka sana kutokana na Uongozi wako. Lakini kabla ya hapo Mheshimiwa Rais utakumbuka mimi nilikuwa Waziri wa Nchi chini ya Ofisi yako, tumefanya kazi wote miaka minne na ilikuwa ndiyo nafasi yangu ya kwanza kuwa Waziri, Wewe ndiyo umenifundisha kuwa Waziri, kwa hiyo kama kuna werevu nilionao basi unatokana na mikono yako na hii nitakwenda nayo kaburini kwangu,” amesema Makamba.